Yanga wanaomba uchaguzi wao wa viongozi uliotangazwa, usogezwe mbele.
Wazee wa klabu ya Yanga, umeomba mchakato wa uchaguzi mkuu wa timu hiyo kusogezwa mbele hadi Julai 5, mwaka huu huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ligomea maombi hayo.
Yanga awali, iliagizwa na TFF, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuanza mchakato huo wa uchaguzi Mei 5, mwaka huu siku ambayo zoezi la utoaji fomu kwa wagombea likianza.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa timu hiyo, Yahaya Akilimali alisema wanaheshimu vyote vinavyosimamia soka na michezo ambavyo ni TFF na BMT ambavyo wangependa kushirikiana navyo kwa manufaa ya klabu yao, lakini wameviomba vyama hivyo kusogezwa mbele uchaguzi huo.
Akilimali alisema, sababu inayowafanya kuomba uchaguzi usogezwe mbele ni vita kubwa ya kupambana kutetea taji lao la Ubingwa wa ligi kuu, Fainali ya FA na Kombe la Shirikisho Afrika (Caf) walipangwa kuvaana na Esperanca ya Angola kati ya Mei 6-8, mwaka huu.
Aliongeza kuwa, kwa hatua hii ya ligi kuu iliyofikia ni ngumu, hivyo wanatakiwa kuzielekeza nguvu zao kwenye ligi kuhakikisha wanafanikisha malengo yao waliyojiwekea kwenye msimu huu.
“Kwa hatua hii tuliyofikia ya ligi kuu, tunahitaji mshikamo na umoja ndani ya timu yetu ya Yanga na siyo kutengana kwa kutengeneza makundi ya upinzani au kuanza kuonyesheana vidole.
“Kama mnavyojua mechi zenyewe zimebaki tano tu za kumaliza ligi kuu, hivyo tunawaomba TFF na BMT kama wanaosimamia soka na michezo kwa pamoja, tunawaomba wasogeze mbe mchakato huu wa uchaguzi wa Yanga,” alisema Akilimali.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Uchaguzi wa TFF, Aloyce Komba kuzungumzia hilo alisema “Kabla maombi hayo hayajafika kwenye meza yangu, ningewaambia tu hao Yanga, hilo suala halipo na tarehe ya uchaguzi haitabadilika.
“Yanga ratiba hiyo wanaijua vizuri kwa sababu tulishamtaarifu katibu wao Baraka (Deudedit), hivyo tunashangaa hayo mengine yanatoka wapi, tunawaambia kuwa wao wanatakiwa wajipange vizuri kwa kucheza mechi za ligi kuu, Fainali ya FA na michuano hiyo ya kimataifa.
“Sitaki kutumbuliwa na mimi kama hao viongozi wengine wanavyotumbuliwa, serikali ipo makini hivi sasa katika masuala haya,” alimalizia Komba.
0 COMMENTS:
Post a Comment