YANGA |
Na Saleh Ally
WAKATI Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-16 inaanza, mikoa miwili tu ya Tanga na Dar es Salaam ndiyo ilikuwa imeweka rekodi ya juu ya kuwa na timu tatu zinazoshiriki ligi hiyo.
Wakati ligi hiyo inafikia tamati, timu tatu za Dar es Salaam zilikuwa zinashika nafasi ya kwanza tokea juu, yaani moja ambaye ni bingwa, mbili na tatu.
Pia wakati ligi inafikia tamati, timu tatu za Tanga zilikuwa zinashika nafasi tatu za mkiani, yaani 14, 15 na 16. Kwa kifupi unaweza kusema, zote kutoka Tanga, zimeteremka daraja!
Hakuna hata mmoja anayeweza kusema Tanga hawajui mpira, mkoa wenye historia kubwa katika soka nchini na mchango wa Coastal Union na African Sports unajulikana.
African Sports wamekaa nje ya ligi kuu kwa zaidi ya miaka 20. Mtoto aliye chuo kikuu sasa, tangu anazaliwa hadi alipo, hakuwahi kuisikia ikicheza ligi kuu.
Imerejea, msimu mmoja imeporomoka. Coastal Union kama wanavyojisifia baadhi ya mashabiki wao, wao ni mabingwa wa kupanda na kushuka, huenda wameiambukiza na Mgambo Shooting ambayo ilionekana ina nidhamu ya juu hapo kabla.
COASTAL UNION |
Yanga, Azam FC na Simba zinabaki namba tatu za juu na timu hizo za Tanga ndizo pekee zimeteremka. Hii ni aibu hata kama Wanatanga wataikataa kwa maandamano, bado itabaki inawahusu.
Lakini unaweza ukashangazwa kama tutatumia takwimu. Yanga ndiyo timu pekee ambayo herufi zake nne za mwisho za jina lake zinafanana na mkoa wa Tanga. Yanga na Tanga ni tofauti ya herufi moja tu.
Lakini kitakwimu zina tofauti kubwa kabisa, maana wakati timu tatu za Tanga zinashuka, kitakwimu zinaonekana zimeshindwa kufikia hata takwimu za juu za timu moja tu ambayo ni Yanga.
Yanga imecheza mechi 30 tu, timu hizo zimecheza mechi 90 kama utachukua mechi 30 za kila timu. Lakini ubora wa ufungaji, ubora wa safu ya ulinzi na mengineyo, Yanga inaonekana iko juu!
Katika mechi 30, Yanga ilifunga mabao 70, timu za Tanga zikamaliza ligi na jumla ya mabao 53 tu, Coastal Union ikiwa imefunga 16, African Sports 13 na Mgambo 24.
Katika mechi 90, timu za Tanga zimepoteza mechi 50, yaani zilipoteza 60% kama utakuwa unatafuta wastani. Yanga ikacheza 30 na kupoteza moja tu ambayo utaipa ubora wa 95%.
Yanga imecheza mechi 30, ikachukua ubingwa kwa jumla ya pointi 73 huku Tanga na timu zote tatu wakafikisha pointi 76 wakikusanya 22 za Coastal Union, African Sports (26) na Mgambo iliyopata 28.
Unaweza kusema haistahili kufananisha. Lakini utaona namna gani timu hizo tatu zilivyokuwa na kiwango cha chini kabisa katika ligi hiyo katika masuala hayo ya kitaalamu kama ufungaji, ulinzi na kadhalika na mfano mzuri ni timu moja kuwa bora kuliko nyingine tatu hata kama zitajumlishwa.
MGAMBO MSIMU WA 2014-15 |
Hii inafanana kabisa na ile ya Ligi Kuu England kwa upande wa pointi. Kwa kuwa timu tatu zilizoshuka daraja za Aston Villa iliyokusanya pointi 17, Norwich (34) na Newcastle (37), jumla ikawa 88. Bingwa Leicester City akakusanya pointi 81 na timu hizo kupewa jina la watatu walioshuka, dhaifu kwelikweli.
Sifa ya udhaifu kwelikweli, bahati mbaya au nzuri inakwenda katika mji mmoja. Hii inachanganya na aibu na itakuwa vizuri Tanga sasa wakubali kujirekebisha ili kuepuka aibu wakati mwingine tena.
Hakuna atakayewakaba na kuwalazimisha hii ni aibu, lakini kila kitu kiko wazi. Roho mbaya, majungu, husda, kujua kupindukia, ubabe usio na tija, yote haya yamewaangusha na msipokubali, yatawalaza kabisa na hamtaamka kisoka.
TAKWIMU:
YANGA TANGA
Pointi 73 76
Shinda 22 18
Poteza 1 50
Mbao (funga) 70 53
Mabao (fungwa) 20 111
0 COMMENTS:
Post a Comment