May 25, 2016


Bado tuzo mbalimbali kwa wachezaji na makocha hazijatoka kwa ajili ya msimu wa 2015/16 uliomalizika wikiendi iliyopita na Yanga kuibuka bingwa lakini tayari wadau mbalimbali wa soka nchini wameonyesha wazi kuvutiwa na tuzo ya kocha bora itue kwa Kocha wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm.

Kila mmoja amekuwa akitaja sababu zake ikiwemo nani anastahili kuwa mchezaji bora wa ligi hiyo ambapo kwa upande huo pia, mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma naye ameonekana kuwakuna wengi kwa kazi aliyoifanya.

Kocha wa zamani wa Geita Gold ya Geita, Selemani Matola ambaye amewahi kuinoa Simba miaka ya nyuma amefunguka kuhusiana na hilo: “Kwa upande wangu, Pluijm anastahili kuchukua hiyo tuzo, ameifikisha Yanga fainali ya FA, ameipa ubingwa na mwisho akaipeleka nane bora ya Kombe la Shirikisho.

“Amefanya kazi nzuri kila mmoja ameiona. Ngoma naye amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga kwenye ushambuliaji, asipokuwepo unaiona Yanga siku hiyo inapata shida kidogo, naye anastahili uchezaji bora ingawa ningependa kuona TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) iache masuala ya uzawa na kumpa mtu anayestahili tuzo kutokana na kazi aliyofanya.”

Abeid Kasabalala ambaye ni katibu msaidizi wa Chama cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza) naye alisema: “Kocha bora ni Pluijm, amefanya vizuri kwa kweli msimu huu, ameisaidia Yanga kila sehemu waliyokuwa wakishiriki na mwishowe wamepata mafanikio, ukiangalia Kombe la FA, Kombe la Shirikisho na hata ubingwa ligi kuu.

“Kwa uchezaji bora nafikiri Kamusoko (Thabani) anastahili sana katika hili, ameisaidia Yanga kwa kiasi kikubwa katikati ya uwanja katika kukaba, kuanzisha mashambulizi na hata pasi zenye madhara, amekuwa bora sana msimu huu.”

Naye kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal ‘Bilo’ aliitupa karata yake kwa Pluijm huku akitaja vigezo vinavyoshabihiana na Matola na Kasabalala na kwa upande wa mchezaji bora akamtaja Ngoma, hasa alivyohusika katika kuchangia mabao mengi aliyofunga Mrundi, Amissi Tambwe aliyeibuka mfungaji bora kwa kutupia mara 21.

“Ngoma anafaa kuwa mchezaji bora msimu huu, amekuwa tishio na msaada mkubwa kwa Yanga tangu mwanzo wa ligi mpaka mwisho. Hata ukiangalia upande wa mabao, yeye mwenyewe kafunga mengi lakini pia amesaidia mno kumpikia mabao Tambwe msimu huu, msaada wake ulikuwa mkubwa mno,” alisema Bilo.


Pia kumekuwa na minongono kuwa tuzo ya kipa bora inaweza kwenda kwa Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye amefanya kazi kubwa msimu huu, huku tuzo ya mfungaji bora ikienda kwa Tambwe aliyefunga mabao 21.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV