May 25, 2016


Kwa mara ya kwanza, beki wa kulia wa zamani wa Simba, Hassan Kessy leo ataonekana kwenye jukwaa la Yanga huku akipanga kuonana na Kocha Mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans van Der Pluijm.

Beki huyo, anatarajiwa kuonekana kwenye jukwaa la Yanga leo wakati timu yake hiyo mpya ikiwa inavaana na Azam FC katika mechi ya fainali ya Kombe la FA.

Kessy alisaini mkataba wa kuichezea timu hiyo wiki mbili zilizopita mara baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu kumalizika Simba na kuwa mchezaji huru. Alisaini Yanga kwa dau la Sh milioni 40, huku akilipwa mshahara wa Sh milioni mbili.

Kessy amesema amepanga kutoka nyumbani kwao Morogoro leo asubuhi na kufika Dar mchana tayari kwa safari ya kuelekea uwanjani kushuhudia fainali hiyo.

Kessy alisema, awali alizoea kukaa jukwaa la Simba kwenye timu aliyokuwa anaichezea, lakini leo atakuwepo kwenye jukwaa la upande wa Yanga ambalo ameandaliwa na mashabiki wa timu hiyo.

Aliongeza kuwa, mara baada ya mechi hiyo kumalizika, amepanga kukutana na benchi hilo la ufundi linaloongozwa na Pluijm na msaidizi wake Juma Mwambusi kwa ajili ya kuzungumza nao kwa mara ya kwanza.

“Nimepokea simu nyingi kutoka kwa mashabiki wa Yanga wakinitaka niende Uwanja wa Taifa kwenye fainali ya FA kati Yanga na Azam, hivyo baada ya kupokea maombi hayo, nimepanga kuwepo uwanjani katika mechi hiyo.

“Nilipanga nije huko leo (Jumanne), lakini imeshindikana na kubanwa na program ya mazoezi, hivyo nitakuja kesho (leo) asubuhi nitafika huko mchana na baadaye kuelekea Taifa.

“Hivyo kwa mara ya kwanza nitaonekana kwenye jukwaa la Yanga katika mechi hiyo, nimepanga kuiangalia mechi hiyo ili kujua mfumo na aina ya uchezaji wanayoitumia Yanga ili mara nitakapojiunga nayo nisipate tabu, pia nitakutana na kocha baada ya mechi hiyo kumalizika,” alisema Kessy. 


Mechi hiyo itakayojaa upinzani mkubwa, itachezeshwa na mwamuzi, Israel Mujuni Nkongo atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza, Soud Lila wa Dar, huku Frank Komba akiwa mwamuzi wa akiba na Kamishna wa mchezo atakuwa Juma Mgunda wa Tanga.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic