Straika nyota wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, leo atakuwepo uwanjani wakati timu hiyo ikivaana na Azam FC katika fainali ya Kombe la FA, lakini kubwa zaidi ameahidi kuipa mataji mbalimbali likiwemo hilo.
Yanga inatarajiwa kuvaana na Azam katika fainali hiyo ya FA itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mchezo unatarajiwa kujaa upinzani mkubwa.
Mrundi huyo, tayari ameiwezesha timu hiyo kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, huku akiipeleka Yanga hatua ya makundi ya Nane Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu. Tambwe alitokea Simba iliyositisha mkataba naye kwenye usajili wa dirisha dogo msimu uliopita.
Tambwe alisema katika mechi zote atakazocheza, atahakikisha anatimiza majukumu yake ya kufunga mabao ili aiwezeshe timu hiyo kutwaa mataji mbalimbali, ukiwemo ubingwa wa leo.
Tambwe alisema, hiyo ndiyo kazi yake, kufunga mabao kuhakikisha anaipa mafanikio timu yake inayofundishwa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm na Juma Mwambusi.
Aliongeza kuwa, pia ataendelea kufunga mabao ili aendelee kuchukua ufungaji bora kwenye kila mashindano baada ya kutwaa mara mbili kwenye misimu miwili tofauti ya ligi kuu msimu wa 2013/2014 na 2015/2016.
“Kati ya vitu ambavyo vinanipa furaha, basi haya mafanikio ninayoyapata nikiwa ninaichezea Yanga, kiukweli nafurahi sana kuiwezesha timu yangu kutwaa taji la pili la ubingwa wa ligi kuu.
“Hivyo nimepanga kuendelea kuipa mafanikio zaidi timu yangu ya Yanga pamoja na mimi mwenyewe kupata mafanikio kama haya unayoyaona ya kuchukua ufungaji bora msimu huu,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment