MAXIME |
Huku Simba na Yanga zikiendelea kufanya mawindo ya usajili wa msimu ujao, imebainika kuwa zaidi ya wachezaji saba wa kikosi cha kwanza cha Mtibwa Sugar wamemaliza mkataba wa kuitumikia timu hiyo.
Mtibwa iliyomaliza nafasi ya tano msimu huu ikiwa na pointi 50, tofauti ya pointi 23 na mabingwa Yanga wenye 73 imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara kuwa wachezaji wake mahiri wanahitajika na vigogo wa ligi hiyo, hivyo kumalizika kwa mikataba yao kwa mkupuo wakati huu kunaweza kuibua hofu ya Mtibwa kuwa na timu dhaifu msimu ujao.
Wachezaji wanaomaliza mikataba hiyo ni pamoja na mabeki wawili wa kati waliounda safu ngumu ya ulinzi msimu huu ya Mtibwa, Salim Mbonde na Andrew Vincent ‘Dante’. Kazi yao imeifanya Mtibwa kushika nafasi ya tatu kwa timu zilizoruhusu mabao machache zaidi kwa kufungwa mabao 21 pekee.
Katika hilo Simba inaongoza ambapo ilifungwa mabao 17 tu ikifuatiwa na Yanga ambao nyavu zao zilitikiswa mara 20 katika mechi 30.
Ukiachana na mabeki hao, wengine waliomalizana na Mtibwa ni kipa Said Mohammed ‘Nduda’, beki wa pembeni, Shaban Majaliwa, Shabani Nditi na kiungo wa zamani wa Simba na Kongsvinger ya Norway, Henry Joseph.
Wengine ni viungo wanaozitoa udenda timu nyingi Bongo kutokana na umahiri wao uwanjani wakiongozwa na Mohammed Ibrahim, Yassin Mzamilu na Ibrahim Rajabu ‘Jeba’ aliyeanza kuvuma tangu akiwa kwenye kikosi cha vijana cha Azam FC takribani misimu mitano iliyopita.
Upande mwingine wachezaji kama Hussein Javu wa Yanga, kipa Hussein Shariff ‘Casillas’ na Boniface Maganga wa Simba wanaelezwa kumaliza mikataba ya kuichezea timu hiyo kwa mkopo hivyo nao wataangalia fursa nyingine.
Alipotafutwa kocha wa timu hiyo, Mecky Maxime kulizungumzia suala hilo, alisema kwa sasa hawezi kusema chochote kutokana na kutojua hatma yake ndani ya kikosi hicho kwani naye tayari ameshamaliza mkataba wa kukinoa kikosi hicho.
“Siwezi kuzungumza sana katika hilo kwa kuwa mimi pia nimemaliza mkataba wangu na sijajua itakuwaje lakini pamoja na hayo, Mtibwa inafahamika kwamba hata iweje msimu ujao lazima kutakuwa na wachezaji wengine wazuri na timu itasimama tu,” alisema Maxime nahodha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment