June 24, 2016

OMOG

Na Saleh Ally
NDANI ya siku mbili tatu, Simba itakuwa imepata kwa uhakika kabisa au kumtangaza kocha wake mpya ambaye atachukua nafasi ya Dylan Kerr.

Kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu, Simba imekuwa chini ya kocha msaidizi ambaye ni kocha mkuu wa muda, Jackson Mayanja raia wa Uganda.

Hakika Mayanja alijitahidi, pamoja na kwamba alikutana na magugu ya nidhamu mbovu ndani ya Simba, lakini alionyesha msimamo wake na kila mmoja alijua kocha huyo alikuwa akitaka kitu gani.

Wachezaji wa Simba ni kati ya wale wanaoongoza kwa ‘kudekezwa’, hasa msimu uliopita. Maana walikuwa ni wale wasiofanya makubwa lakini walipenda kutukuzwa kwa sifa zinazozidi uwezo wa walichonacho.

Wachezaji wengi wa Simba walivimba majibu mapema kabisa. Walianza kujiona hakuna wa kuwalinganisha au wao ni watu wa kiwango kingine, jambo ambalo lilikuwa ni upuuzi mkubwa kuliamini.

Safari hii, Simba inatafuta kocha kwa umakini mkubwa. Kwa kuwa Kocha Sellas Tetteh raia wa Ghana anaonekana kama anaona Simba ni ndogo kwake, huenda nafasi ikawa kubwa na uhakika kwa Joseph Omog raia wa Cameroon ambaye tayari anayajua mazingira ya Tanzania kwa kuwa mwaka 2014, aliiongoza Azam FC kubeba ubingwa wa Tanzania Bara.

Wakati Simba inasubiri kuwa na uhakika wa kocha wake mpya, mimi nimeamua kusema ambayo ninaamini ni sahihi ili kuwasaidia Simba kama watayaamini na kuyafanyia kazi.
Uliza duniani kote kupitia mchezo wa soka au mingine kama kuna kocha amekuwa akitegemea mawazo ya mwajiri wake kupata mafanikio, haijawahi kutokea.

Kocha ndiye mtaalamu, vizuri apewe nafasi ya kufanya kazi yake kama ambavyo inatakiwa. Ndiyo maana makocha wengi wakifanikiwa katika klabu mbalimbali za Ulaya husifiwa kwa ubora wa kazi zao, wakifeli basi mara moja wanatimuliwa.

Hapa nyumbani, kocha akifanikiwa, viongozi nao hutaka kusifiwa kwa kuwa wanajua walikuwa wanashiriki hadi kupanga kikosi kwa kuwa wao ndiyo mabosi wa kocha. Lakini kikosi kikiboronga, basi mambo yanakuwa kama Ulaya tu, kocha anatimuliwa kwa kushindwa kufanya kazi yake vizuri.

Ukizungumza na kiongozi yeyote wa Simba, atakuambia kwamba hahusiki na upangaji wa kikosi wala hajawahi kumueleza kocha suala hilo, ni uzushi mtupu.

Makocha kadhaa wamekuwa wakilalamika kwamba kuna hiyo tabia na viongozi wako ambao wanapita kona na kuwasiliana na makocha wakitaka mchezaji fulani asicheze na mwingine acheze, jambo ambalo si sawasawa hata kidogo.

Ninaamini wako viongozi wengi watiifu ndani ya Simba ambao wako makini, lakini wako ambao hawako makini na wanaweza kuwa wakifanya hivyo kwa maslahi yao binafsi, kama wanajua sana, watafute timu Ligi Kuu Bara, wafundishe.

Angalia, haujawahi kusikia kocha kutoka Yanga akilalamika kwamba uongozi unamuingilia katika kazi yake ya upangaji kikosi. Sasa jiulize, vipi iwe Simba tu?

Kocha wa Yanga ndiye bosi hasa wa benchi la ufundi. Ninaamini hata Yanga wamekuwa wakimshauri lakini lazima tukubali, ushauri nao una kiwango chake. Si sawa kuvuka mipaka na ukageuka na kuwa agizo kwa kuwa anayesema anakuwa ni bosi wa mwalimu.

Mwalimu ni mtaalamu aliyesomea kazi yake, lakini kawaida inamtaka kuunda kikosi ambako analazimika kutumia akili kwa kusoma kundi la wachezaji wake, kuwagawanya na baadaye kuwajumlisha baada ya kuwa amemsoma na kumtengeneza mmoja baada ya mwingine ili kuunda kikosi imara.

Hii haiwezi kuwa kazi rahisi au inayoweza kwisha kwa siku mbili tu na ianze kuzaa matunda. Vizuri pia kwa wanaotoa ushauri, uwe ni ule wenye maslahi ya timu na si maslahi binafsi, kitu ambacho mwisho kinajenga hisia za faida ya matamanio ya kila mmoja anavyojifikiria. Mwisho wake, Simba inaendelea kuwa ya tatu, kila mwisho wa msimu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV