June 24, 2016




Na Saleh Ally
SHIRIKISHO la Soka la Afrika (Caf), limempa nafasi mwamuzi Janny Sikazwe kuamua mchezo kati ya mabingwa wa Tanzania, Yanga dhidi ya TP Mazembe, hii ni mechi ya Kombe la Shirikisho hatua ya makundi.

Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumanne na inasubiriwa kwa hamu kubwa.

Caf imewatangaza waamuzi wasaidizi kuwa hivi; washika vibendera ni Berhe O’Michael wa Eritrea na Wellington Kaoma wa Zambia pia atakuwa line 2. Kamishna ni Celestin Ntangungira anayetokea Rwanda. Pia kutakuwa na Mratibu Mkuu Maalum wa mchezo huo kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza.

Vizuri kabisa Yanga ikamjua Sikazwe ni mtu wa aina gani. Huyu ni mwamuzi aliyeingia kwenye fainali ya waamuzi bora wa Afrika katika tuzo za Glo-Caf zilizofanyika nchini Nigeria, mwaka jana akichuana na waamuzi wengine wa juu barani Afrika kama Alioum Neant wa Cameroon, Eric Arnaud Otogo-Castane (Gabon), Ghead Zaglol Grisha (Misri) na Bakary Papa Gassama wa Gambia aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo.


Sikazwe ni mwamuzi mzuri bila shaka, mwenye mkwara kwa wachezaji na amekuwa akiutumia urefu wake kuonyesha hana hofu na hajali.

Lakini rekodi zinaonyesha marefa bora wamekuwa wakitumiwa na timu kubwa na wakati mwingine wadau wa karibu wa Caf kuziangamiza timu ndogo na kuzitetea kubwa barani Afrika.

Timu kubwa kama Al Ahly, TP Mazembe, Esperance na nyingine kubwa zimekuwa zikibebwa mara nyingi hasa zinapoonekana zimezidiwa. Inaonekana ni siri, lakini hakuna anayeweza kukataa kwamba kwenye soka kuna rushwa na timu zenye fedha nyingi hutumia nguvu zao kifedha.

Hakuna anayeweza kukataa, pia Yanga itaingia kwenye dimbwi la dharau inayopewa ukanda wa Afrika Mashariki kuonekana hauna kitu. Vizuri timu za Kaskazini na zile za Magharibi au Afrika ya Kati kama TP Mazembe zifanye vizuri zaidi.

Timu za ukanda wa Magharibi, Kaskazini na hata Kati, kweli ni bora, lakini pia zinafanikiwa kutokana na uwezo mkubwa wa kuzibeba figisu za nje ya uwanja. Waamuzi ni kati ya “Watumwa wa wafalme” ambao wamekuwa wakisaidia.

Hatuwezi kutanguliza lawama kwa Sikazwe lakini akikanyaga ardhi ya Tanzania, wamfikishie salamu kwamba kinachotakiwa ni haki bin haki ili Yanga ikifungwa kwa haki, Watanzania wajue kweli iliteleza na uwezo wake ulipungua sehemu fulani.


Katika mechi nyingi za TP Mazembe alizocheza Sikazwe zinaonyesha timu hiyo ilipoteza moja tu kwa kufungwa bao 1-0 na Al Hilal mjini Khartoum, Sudan. Hiyo ilikuwa Mei 16, 2014.

Ukiachana na hivyo, mechi zote zilizobaki TP Mazembe ilishinda na nyingi kumekuwa na lawama kubwa, kwamba alionekana kuwabeba wakubwa hao kama ambavyo nimeelezwa.

Katika soka, suala la lawama limekuwa kama ada. Waamuzi wengi wamekuwa wakilitumia kama nafasi ya kuangamiza wengine kwa kuwa wanaamini lazima watu watalaumu, hivyo wanataka kuonyesha ni lawama tu, wakati wao wanakuwa wametekeleza malengo mengi.

Kumekuwa na taarifa hata kitengo cha upangaji waamuzi kimekuwa kikizidiwa nguvu na klabu kubwa, kwamba mwamuzi fulani achezeshe mechi zao.

Mfano msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa, Sikazwe alichezesha mechi tatu za TP Mazembe, ikashinda mbili dhidi ya Stade Malien (2-1) na Moghreb (5-0), zote ikiwa nyumbani Lubumbashi kabla ya kufungwa 1-0 na Al Hilal, Sudan.

Sikazwe anaonyesha ni ‘mbaya’ kwa kadi za njano. Ni anayeonya kwa maneno sana, halafu ukizidi njano inafuatia. Wakati mwingine ni mbabe na mgumu wa kutoa kadi nyekundu.

Msimu uliopita kwa ligi ya kwao Zambia na mechi zote za kimataifa kuanzia zile chini ya Caf na Fifa, alitoa kadi za njano 214, nyekundu 6. Alichezesha jumla ya mechi 63 za kimataifa.
Msimu huo, Sikazwe alitoa jumla ya penalti 9. Hii inaonyesha mtu akifanya ujinga katika eneo la 18, basi ajue ‘ameiharibia’ timu yake.

Kwa Wazambia, DR Congo ni kama nyumbani, ninaamini Sikazwe ataonyesha umahiri wake na kuchezesha kwa haki kwa kuwa Yanga inaweza kuwa na nafasi ya kufanya vema kama uamuzi hautakuwa sehemu ya kuivuruga.
Vizuri watakaofika Uwanja wa Taifa siku ya mchezo, washuhudie kwamba kama Yanga imefanya vizuri bila ya kubebwa na mwamuzi. Ikifanya vibaya, basi isiwe kwa kuonewa na Sikazwe kwa vile vigezo nilivyovitaja pale juu.

TAKWIMU:
Penalti:    9
Kadi nyekundu:      6
Kadi njano:    214

*MECHI ZA KIMATAIFA 63

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic