June 15, 2016


Na Saleh Ally
WAZIRI wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Geroge Simbachawene ametangaza rasmi kuzuiwa kufanyika kwa Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi (Umitashumta) na ule wa shule za sekondari (Umisseta).

Michezo ya Umisseta ilipangwa kufanyia kuanzia jana hadi Juni 22 jijini Mwanza, ni siku tisa. Halafu ile ya Umitashumta ingefanyika kuanzia Juni 25 hadi Julai 5, jumla ni siku 10.

Simbachawene amesema wameamua kusitisha michuano hiyo ili kuweza kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli kuhusiana na suala la madawati mashuleni. Wanataka kutekeleza kwa wakati agizo lake la kila mwanafunzi kuwa ameketi kwenye dawati ifikapo nwishoni mwa mwezi huu.

Waziri Simbachawene hajui kama wachezaji nyota wa Tanzania walipatikana katika Umitashumta na Umisseta. Iliposimamishwa na Waziri wa Elimu, Joseph Mungai wakati huo, ilikuwa ni kuiua michezo na madhara yake tumeyaona miaka nenda rudi. Serikali ya awamu ya nne ilielewa kosa lililofanyika katika awamu ya tatu, ikairejesha michezo mashuleni.


Simbachawene, ameizika rasmi. Yeye anasema itafanyika itakapotajwa tena, huenda mwakani lakini alichokifanya ni kuonyesha ni kiasi gani michezo imewekwa kama ‘spea tairi’ katika nchi hii, kila kitu kinakuwa wazi, haitakuwa na maendeleo.

Nawakumbusha Dua Said aliyeng’ara Simba, leo ana miradi yake na anaendesha maisha lakini hakuwahi kufika chuo kikuu. Soka ilimtoa kimaisha leo anaweza kuishi vizuri kuliko wahitimu wa chuo kikuu.

Tunawajua wachezaji wengi Watanzania ambao wana ajira zao kwa sasa, wanalipwa mishahara ya Sh milioni moja na zaidi kwa mwezi na serikali inaingiza kodi, lakini walianzia kwenye mashindano hayo ya mashule.

Nyota wa taifa hili, mfano Edibily Lunyamila, kwenye kikapu Ramadhani Dullah, Nteze John Rungu aliyeng’aa baadaye Pamba na Simba, hawa wote ni zao la Umisseta na Waziri Simbachawene halijui hili, ameamua kwa kuwa anataka kutimiza agizo la rais la madawati.

Sitaki kusema agizo la madawati ni baya, lakini ninaona ni uamuzi wa hofu, kwa kuwa Waziri Simbachawene haujui umuhimu wa michezo, hajui tulivyoipigania irudishwe na huenda hajui michezo ni somo jingine muhimu na nyenzo muhimu ya afya bora.


Ninaamini anaona michezo ni michezo kwa ajili ya kucheza. Anasahau ni ajira na chanzo kikubwa cha ajira, ndiyo maana wachezaji ambao hawajafika chuo kikuu hapa nyumbani, wanalipwa fedha nyingi kuliko wafanyakazi waliohitimu vyuo vikuu.

Serikali nayo inafaidika na kodi kupitia michezo kwa kuwa mishahara mikubwa na kodi inayopatikana ni nyingi. Sasa vipi uue michezo ili ufanikishe kutengeneza madawati?

Kwani Simbachawene haumizwi na hili? Kama angekuwa ameagizwa ningeanza kuwaza ameshindwa vipi kumshauri rais kwamba michezo ni ajira, michezo ni chanzo cha kodi na tunapaswa kuanza kuwakuza na kuwalea au kuwaona vijana wengi wakiwa shuleni kwa kuwa haitatokea siku mchezaji akakua kama mbuyu, lazima apitie hatua hizo.

Niwe mkweli, nimeumizwa sana kuona kwa mara nyingi michezo inarudishwa shimoni na serikali ambayo imekuwa haiko tayari kuisaidia michezo na huku viongozi wake wakiwa ni sehemu ya wanaofurahia kwa kiasi kikubwa inapotokea wanamichezo wakapata mafanikio kiduchu kabisa.

Serikali itafakari, ilichofanya imekurupuka. Huenda wako wanaohofia kusema kwa visingizio vingi tu. Lakini mimi siwezi kuwa mwoga kwa kuwa hii ndiyo nchi yetu sote, tunapaswa kupigania kila kilicho sahihi.

Alichofanya Waziri Simbachawene si sahihi hata kidogo na inaonyesha ni uamuzi uliojaa uoga. Na kama itakuwa ni uamuzi kutoka juu serikalini, pia si sahihi kwa kuwa ni kuidharau na kuirudisha nyuma michezo huku mkidhoofisha vipaji vya vijana.

Msitake kutushawishi kuwa kila mtoto atakayetokea shule ya msingi na baadaye sekondari atakwenda chuo kikuu. Wengine wataishi kwa vipaji vyao baada ya hapo, hivyo ni vizuri kuviheshimu vipaji. Kwa kuwa serikali haionyeshi mapenzi navyo katika kuvilea, basi vizuri ikaheshimu mashindano machache kama hayo iliyoyasimamisha.


Serikali haina mpango mkakati wowote wa kuendeleza michezo kwa maana ya kujenga vituo vya michezo. Kuendeleza vipaji na vitu vingi vinaendeshwa na taasisi tu.

Kama nilivyoeleza awali, kwenye mafanikio serikali kwa kuwa ndiyo baba inajumuika. Sasa imeamua kuziba mfereji tena wa ukuzaji na endelezaji wa vipaji vya michezo ambavyo baadaye vinaweza kujitegemea katika suala la ajira na kuipunguzia serikali kazi. Sidhani kama kulikuwa na upembuzi yakinifu katika hili au kwa kuwa ile ‘watasema watachoka’ linaonekana ni jambo la kawaida tu kwa kipindi hiki. Nasisitiza, kilichofanyika si sawa hata kidogo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV