June 15, 2016


Wakati Yanga ikielekea Uturuki kujiandaa na mchezo wao dhidi ya MO Bejaia ya Algeria katika Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa timu hiyo, Mdachi, Hans van Der Pluijm, amewatahadharisha wachezaji wake maadui wao watatu wakubwa katika michuano hiyo.

Upelelezi uliofanywa na Pluijm kupitia njia mbalimbali zikiwemo DVD za mechi za wapinzani wake alionao Kundi A wanaoungana na Bejaia, zikiwemo TP Mazembe (DR Congo) na Medeama (Ghana), umebaini mambo hayo na kusisitiza kuwa kama watayafanyia kazi basi nusu fainali inawahusu.

Pluijm amesema kuwa ukiachana na adui wa kwanza ambao ni timu pinzani lakini pia kuna waamuzi na mwisho ambao ni mashabiki na kupigana na maadui wote hao jukumu hilo wanalo wachezaji wake wakiwa uwanjani na tayari ameshawaambia nini cha kufanya kuwamaliza maadui hao.

“Kuhusiana na wapinzani wetu, nimegundua kuwa wote wanacheza kwa kushambulia muda wote wakiwa kwao, hilo nimewaeleza wachezaji wangu nini cha kufanya kwa kutumia falsafa ya njia nzuri ya kuzuia ambayo ni kushambulia.

“Adui mwingine wanayepaswa kumtambua na kucheza naye kwa umakini ni mwamuzi, wengi huwa upande wa mwenyeji kwa hiyo wajue hakuna mtetezi zaidi ya kujichunga na kupambana kweli. Wa mwisho ni mashabiki wao.

“Hawa muda wote wanashangilia kwa kuvuruga akili za wachezaji, ili kuwatuliza ni kuifunga timu yao mapema. Nimewaona hawa mashabiki mara kadhaa wakianza kufungwa wanapoteza morali, hiyo itatupa uhuru wa kucheza kwa kujiamini kwa maana tumedhibiti jukwaa.”

Yanga inatarajiwa kuingia Algeria siku mbili kabla ya mchezo wao na Bejaia utakaopigwa Juni 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Unite Maghrebine. Yanga imefika hatua hiyo baada ya kuifunga Esperanca Sagrada ya Angola kwa jumla la mabao 2-1 kwa matokeo ya jumla.

CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV