Na Saleh Ally
UWANJA unaotumiwa na Mouloudia Olympique de Bejaia au Mo Bejaia unajulikana kwa jina la Unite Maghrebine, uko katika Mji wa Bejaia.
Kutoka mji mkuu wa Algeria uliotwao Algiers hadi Bejaia ni umbali wa Kilomita 228, umbali wa saa 3:30 kwa gari kwa mwendo chini ya sheria za nchi ya Algeria.
Usiku wa kuamkia keshokutwa, Yanga watakuwa uwanjani tayari kuwavaa wenyeji wao Bejaia katika mechi yao ya kwanza ya kihistoria ambayo kamwe haiwezi kuwa rahisi kama ambavyo mashabiki wanaifikiria.
Tunaiita mechi ya Kihistoria kwa kuwa gumzo lilikuwa ni Yanga kufuzu katika michuano hiyo lakini sasa ni kuanza kushiriki rasmi na kucheza kwa mara ya kwanza.
Kinachotakiwa kikubwa ni Yanga kuanza kucheza michuano hiyo na kufanya vizuri. Mechi ya kwanza inaweza kuwa dira nzuri ya mwendo wa Yanga kwa ajili ya kujenga hali ya kujiamini katika mechi nyingi zinazofuatia.
Ukiangalia kishabiki, unaweza kuona Yanga wana kazi rahisi sana kwa kuwa Bejaia ambayo imeanzishwa mwaka 1954 ni changa hata kwao ambao walianzisha klabu yao mwaka 1935. Lakini ukweli unaonyesha hivi, Bejaia wana kiu kali ya maendeleo na litakuwa kosa kubwa kuanza kuwachukulia kwa udogo au wenye kasi ndogo kama Bajaj unapolinganisha na gari lenye mwendo kasi kama Range Rover Vogue.
Kubali kwamba, Mo Bejaia wanataka kufanya vema zaidi na lazima watataka kuimaliza Yanga hasa nyumbani. Ndiyo maana licha ya kuwepo kwa timu kubwa na maarufu za Algeria kama USM Alger, JS Kabylie na ES Setif lakini wao wanaendelea kuwa wawakilishi wa nchini hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kitakwimu inaonekana Bejaia ni timu yenye mwendo wa saizi ya kati lakini makini kwenye ulinzi na haifungi mabao mengi sana lakini wastani wake wa ushindi uko juu.
Katika michuano ya kimataifa, hili Yanga wanapaswa kulitazama zaidi. Inaonekana haijapoteza mechi nyumbani na ilifanikiwa kupata ushindi zaidi ya mara mbili ambao unakwenda kuanzia mabao mawili hadi matatu, ikiwa nyumbani imekuwa ikiruhusu mabao machache sana.
Kibaya zaidi, inaonekana ni timu ngumu kuruhusu mabao ikiwa nyumbani, jambo ambalo Yanga watatakiwa kulifanyia kazi sana.
Takwimu zinaonyesha timu hiyo, ilikwenda vizuri kwenye Ligi Kuu ya Algeria ingawa ikakwama katika nafasi ya sita. Lakini pointi kati ya aliye nafasi ya pili na nafasi ya sita ni mbili au tatu tu, jambo ambalo linaonyesha pia ligi ya nchi hiyo ilikuwa na ushindani wa juu kabisa.
Takwimu za uchezaji, zinaibeba sana Mo Bejaia licha ya ligi ya ushindani wa juu wa nyumbani kwao. Ukiangalia, ni nadra sana kucheza mechi mbili bila ya kushinda.
Takwimu zinasema imeweza kucheza mechi tatu bila ya kupoteza na ikacheza mechi tano mfululizo bila ya kupata sare, maana yake ni timu inayochipukia lakini hatari sana.
Yanga hawatatakiwa kuibeza kwa kuwa kufikia hatua hiyo moja ya timu ilizozitoa kwenye Kombe la Shirikisho ni Club African ambayo ndiyo timu yenye mashabiki wengi zaidi nchini Tunisia ikifuatiwa na Esperance halafu Etoile du Sahel.
Ukiachana na hivyo, ndani kuna wachezaji ambao iwe isiwe, Yanga inapaswa kuwa makini nao kwa kuwa rekodi zao kiufungaji katika mechi za nyumbani na hizo za kimataifa wamethibitisha ni watu hatari sana.
Mfano Mohammed Waliou Ndoye raia wa Senegal ambaye anavaa namba jezi 19, huyu ni mtu hatari. Katika mechi nne kafunga mabao matatu, hizi ni zile za Ligi Kuu Algeria lakini zile za kimataifa, mechi nne kafunga mabao mawili. Ninaamini Yanga wamejiandaa zaidi yake kwa kuwa ni mwepesi na hatari kwenye kupiga mashuti.
Bado wana kiungo Zahir Zerdab anayevaa namba 22 mwenye uraia wa Ufaransa pia Faouz Yahaya mwenye namba 10 mgongoni, ni watu hatari ambao rekodi za ufungaji za mabao mawili katika kila mechi nne zinawabeba.
Kitu kingine kizuri kwa Waarabu hao ni kwamba ina wigo mpana wa wafungaji. Niliowataja kama watashindwa kufunga bao kuna akina Soumaila Sidibe raia wa Mali, Ismail Belkacemi ambao wamekuwa mara kwa mara wanapatikana katika listi ya wafungaji.
Kingine wanachopaswa kukumbuka Yanga ni kwamba sehemu ya ulinzi, Mo Bejaia wanaonekana kuwa imara sana. Ni timu yenye mashambulizi machache lakini mazito, lakini haitaki kabisa kufungwa.
Lazima tumwamini Pluijm na wachezaji wa Yanga, lakini lazima tuwakumbushe kama namna hii. Tuwaamini wamejiandaa vizuri lakini umakini ndani ya dakika 90 unapaswa kuwa juu zaidi ya mechi zote walizocheza.
Ugenini kuna ugumu wake, lakini umakini wa juu au zaidi kama ule katika mechi dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola, unahitajika.
TAKWIMU ZA MO BEJAIA:
Cheza mechi bila kupoteza: 1
Kucheza mechi bila kushinda: 1
Kucheza mechi bila kupoteza: 3
Sare za mfululizo katika mechi tano: 1
Kushinda mechi za nyumbani mfululizo: 1
Kucheza nyumbani bila kupoteza mfululizo: 8
Mechi za nyumbani mfululizo bila ya sare: 1
Mechi mfululizo za ugenini bila kushinda: 5
Kucheza ugenini mfululizo bila kupoteza: 2
Ushindi mkubwa 5-1
Kipigo kikubwa 0-2
Wastani wa mabao kwa mechi 2.05
0 COMMENTS:
Post a Comment