July 8, 2016


Baada ya kuibuka kwa sitofahamu ya muda mrefu kuhusiana na ajira ya Kocha Jackson Mayanja kama ataendelea na Simba msimu ujao au la, hatimaye mambo sasa yameanza kukaa sawa na muda si mrefu kocha huyo anaweza kutangazwa kama msaidizi wa kocha mkuu, Joseph Omog kuelekea msimu ujao.

Awali kulikuwa na kikwazo cha kusubiri tamko la Omog kama angependa kuendelea naye au la ambapo hilo likapita na kuibuka jipya la yeye kuamua kati ya ofa ya Simba au Kagera Sugar walikomwita akasaini mkataba wa kuwa kocha mkuu.

Hata hivyo, baada ya mazungumzo ya takriban siku mbili na uongozi wa Simba wakawa wamemalizana kila kitu kasoro kwenye ishu ya mshahara lakini hilo nalo sasa limekwisha na Mayanja ameanza kuhudhuria katika mazoezi ya timu hiyo akisubiri kumwaga wino saa yoyote kutoka sasa.

Makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo mbili ni kumpa kandarasi ya miaka miwili kocha huyo itakayomalizika mwaka 2018, ikiwa sawa na muda anaomaliza mkataba Omog klabuni hapo.

Mayanja alipotafutwa ili kupata ufafanuzi kuhusiana na hilo ambapo alisema:

“Kwa kifupi niseme tu mazungumzo yanaendelea vizuri, nimeona kuna nafasi nzuri ya kuendelea kubaki Simba ukizingatia niliishi na uongozi na mashabiki vizuri tu msimu uliopita ni vizuri ikieleweka hivyo kwa sasa.”


Alipotafutwa Katibu wa Simba, Patrick Kahemele kuzungumzia hilo, hakupatikana. Alipopigiwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe simu yake haikuwa hewani, upande wa Rais wa Simba, Evans Aveva yeye simu yake iliita bila ya kupokelewa.

1 COMMENTS:

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV