July 8, 2016Na Saleh Ally
KUNA mchezo wa kijinga kabisa umekuwa ukiendelea katika Klabu ya Stand United ya Shinyanga ambao kwa hakika unapaswa kukemewa, lakini haiwezekani.

Haiwezekani kwa kuwa mkemeaji naye ameingia ndani ya mchezo huo wa kijinga, hali inayofanya mambo ya kijinga yazidi kuendelea huku watendaji wa mambo hayo wakiamini kila anayewasikiliza na kuwafuatilia ni wajinga kama wao.

Ndani ya Stand United kuna mgogoro ambao sasa unaonekana uko hivi; waanzilishi wa timu dhidi ya wengine ambao wako hapo kuhakikisha wanaikwapua kwa kuwa imepata udhamini wa mamilioni ya fedha kutoka Acacia Gold Mine.

Baadaye nitaeleza ninachokiona kuhusiana na hili namna ambavyo Stand waliokuwa wawakilishi na wanaoubeba Mkoa wa Shinyanga kwa kuwa na timu iliyoanzishwa na wazalendo wa kawaida kabisa yaani wapiga debe wa Stand, sasa inataka kugeuka aibu ya mkoa.


Kilichonikera zaidi na kinachonishangaza kabisa ni jambo hili la kijinga ambalo limo ndani ya mgogoro huo. Hili linahusiana na usajili kwa kuiona Stand United moja inafanya usajili sehemu mbili tofauti na kila upande ukijisifia kwamba wao ndiyo Stand United.

Nitakupa mfano huu, Stand United moja imetangaza kumuongezea Haruna Chanongo mkataba wa miaka miwili. Stand United nyingine imetangaza kumtema kiungo huyo wa pembeni kwa madai haimhitaji!

Ajabu au kitu kibaya zaidi, Stand zote mbili zina wasemaji tofauti na kila mmoja anapata nafasi ya kuzungumza na vyombo vya habari kuelezea maandalizi ya msimu mpya ukiwemo usajili huo mpya.

Kinachokasirisha kabisa ni wasemaji au viongozi wa kila upande kuzungumzia usajili huo kwenye vyombo vya habari hali ambayo hakika inachanganya au kukera hata kuisikiliza kwa kuwa kila mmoja atajiuliza swali hivi; “Hivi ipi ni Stand United hasa?”

Ukiachana na hapo, kinachoudhi zaidi ni vyombo vya habari vyenyewe ni kuwafanyia Stand United hao wawili mahojiano hata bila ya kutaka kuchimba au kujua ipi hasa ni sahihi na kwa nini imekuwa kuna mvurugano huo.

Badala yake, wanapohojiwa watazungumza kuhusiana na uamuzi wao wa kumpa Chanongo miaka miwili, wale wengine watazungumzia wanavyomuacha, imekwisha hiyo, hakuna cha zaidi!


Inaonekana hawa watu wa kila upande hawana cha kufanya au kama wanacho basi lengo lao ni kuiangamiza Stand United na ikiwezekana ni kuufelisha Mkoa wa Shinyanga katika soka kwa faida au hamu na tamaa ya matumbo yao. Hili ni jambo la kijinga kabisa.

Wadhamini wa Stand United, Acacia Gold Mine wametoa udhamini wa zaidi ya Sh bilioni mbili na hicho ndicho kinachowatoa ‘roho’ baadhi ya wale ambao sasa wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanaingia na kuwa sehemu ya Stand United.

Inaonekana kama hawajui wanaumwa nini lakini wanaotaka kuingia si watu wenye aibu hata kidogo, wanajua wazi wanaonekana wanalazimisha kuwa wadau wa Stand United, lakini hawajali kwa kuwa kuna kile ambacho wanakitaka na wenyeji nao wamekuwa wakali wanaendelea kupambana.

Siamini kama wadhamini hao wangeingiza fedha nyingi kiasi hicho kuidhamini timu hiyo huku wakijua kungekuwa na migogoro ya namna hiyo kama ambayo inaendelea sasa.

Kuna uwezekano Stand United imekuwa sasa baada ya kuendelea kubaki Ligi Kuu Bara.  Hivyo kuna suala la uendeshaji kiujuzi linatakiwa, sawa, lakini hao wapya wanaotaka kuingia, vipi wanataka kupora kila kitu kutoka kwa waanzilishi au waliopambana kuifikisha hapo?


Kama wapya wanaona wana akili nyingi sana, basi waanzishe timu yao na kuifikisha hapo. Kama hawawezi wawaheshimu waanzilishi na vema wakakaa pamoja na kuona kipi kinachowezekana ili kuibakiza Stand United kuwa moja kama ilivyokuwa mwanzo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linashindwa kumaliza tatizo hilo mapema kwa kuwa kuna baadhi ya viongozi wake nao wanaonekana wana upande ndani ya sakata hilo la Stand United na hiki ni kitu kibaya kabisa.

TFF itaendelea kujichafua kwa mambo madogo kama haya ambayo baadaye yatajenga ukungu. Vema ikawa na mikono misafi ikiingia katika sehemu kama hizi kuhakikisha inaendesha na kuongoza kwa haki.


Wananchi au wapenda soka wa Shinyanga na Tanzania kwa jumla, hawahitaji hadithi za kijinga kama zinazoendelea sasa, badala yake maendeleo ya soka yenye nguvu moja kupitia kundi moja lenye mapenzi ya kwenda kwa ajili ya maendeleo.

1 COMMENTS:

  1. Hapa nimepata taarifa za kutosha kuhusu mgogoro wa Stand United. Waanzilishi lazima wapewe heshima yao. Inaelekea hao wengine ni njaa yao inawapeleka baada ya kuona udhamini mnono toka kampuni ya Acacia Gold. Inawezekana wale waanzilishi wakakosa "elimu na ujuzi" wa kuendeleza timu, lakini itakuwa ni makosa kuwakabidhi vibaka wasomi ambao wala hawajui timu ilianzia wapi. Hao "wasomi" waingie ndani ya Stand United kwa taratibu na katiba ya club. Uporaji haukubaliwi!

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV