July 15, 2016


Yanga na Medeama ya Ghana ni kesho Jumamosi lakini Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm amewaambia wachezaji wake kuwa anataka kuona muda wote wanacheza kwenye eneo la wapinzani, yaani ni kuchapa, chapa, chapa hadi kieleweke. 

Timu hizo zinakutaka katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo ushindi pekee ndiyo utakaoamsha matumaini ya kusonga mbele.

Pluijm ameyasema hayo alipokuwa katika mazoezi ya timu yake juzi, ambapo alionekana kuwa bize akitoa mbinu za jinsi ya kushambulia.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani, Dar, Pluijm alikuwa akitaka wachezaji wanapokuwa kwenye nusu yao waguse mpira mara moja na kutoa pasi, lakini wanapovuka mstari wa kati wanatakiwa kuwa huru kuuchezea mpira watakavyo huku wakitengeneza nafasi za kufunga.

Zoezi hilo lililodumu kwa takribani dakika 20, lilienda vizuri hali iliyomfurahisha Pluijm ambapo baadaye aliliambia Championi Ijumaa kuwa lazima wafanye hivyo kutokana na kwamba staili hiyo inamlazimu mpinzani wako kukaa zaidi katika eneo lake na kukupa nafasi ya kumshambulia.

“Unapotaka kumshinda mpinzani wako ni lazima umlazimishe abaki kwenye eneo lake ndiyo maana nataka kwenye mechi tucheze zaidi kwenye eneo la wapinzani kuliko kwetu.

“Sitaki kuona tunacheza sana kwetu na badala yake muda wote tuwe kwa wapinzani.

“Lakini pia nataka tufanye kama ilivyokuwa kwenye ligi, muda mwingine tulikuwa tunaanza kufungwa lakini tunajipanga na kurudisha na hatimaye kuibuka na ushindi, sasa hali hiyo nataka pia tufanye kwenye michuano hii ya kimataifa,” alisema Pluijm.

Wakati huohuo, mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma amedai kuwa hataki kuona wala kusikia suala la kufungwa katika mchezo huo.


“Hatujafunga na hatuna pointi yoyote jambo ambalo siyo zuri kwetu, nafikiri tukifanya vizuri katika mechi hiyo itatufanya tufufue matumaini. Tutapambana kwa muda wote,” alisema Ngoma.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV