July 16, 2016


Simba wanapenda siri bana ee! Safari hii wamefanya siri hadi kwa makocha na wachezaji wao walio kambini Morogoro.

Maana viongozi Simba wamefanya tukio moja la kimafia kidogo, kwani ilimsafirisha straika Ndjack Anong Guy Seuges raia wa Cameroon usiku kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ilipo kambi yake na jana asubuhi akaonekana mazoezini.

Hakuna mchezaji wa Simba aliyefahamu ujio wa straika huyo zaidi ya asubuhi kumuona wapo naye mazoezini na kuzua maswali vichwani mwao lakini wakaambiwa: “Huyu kaja kujaribiwa.”

Mmoja wa wachezaji wa Simba waliopo kambini Chuo cha Biblia cha Highlands, Morogoro aliliambia Championi Jumamosi kuwa: “Hadi usiku tunalala hatukuwa tunafahamu kama kuna mchezaji anakuja, lakini asubuhi tukashtukia mtu mpya mazoezini.”

Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema: “Ujio wa Mcameroon huyu ni mwendelezo wa kusaka wachezaji, atafanyiwa majaribio kuona kama anafaa.”

Kocha Joseph Omog na msaidizi wake Jackson Mayanja walimpokea Seuges na kuanza kutazama uwezo wake na watatoa majibu siku chache zijazo. Mayanja alikiri kumpokea Seuges.

Seuges ameungana na wachezaji wengine wa kigeni wanaowania kusajiliwa Simba wakiwemo Musa Ndusha na Janvier Bukungu (wote kutoka DR Congo), Muivory Coast, Blagnon Fredric na Mzimbabwe, Method Mwanjali.

“Kwa jinsi ninavyowaona wote wanaweza kubakia kwa sababu wanaonyesha uwezo mzuri uwanjani lakini jibu kamili tutalijua kesho (leo) au keshokutwa (kesho) Jumapili baada ya makocha kumaliza kazi yao,” alisema bosi huyo wa Simba.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV