August 24, 2016

Na Saleh Ally, Bilbao
BILBAO iko Kaskazini mwa nchini ya Hispania, si mbali na mpaka wa Ufaransa. Ni sehemu iliyoendelea ingawa mwonekano wake ni kama sehemu fulani isiyo na tafrani, utulivu uko juu.

Watu wa Bilbao hasa eneo la Saint Mammes, wanajivunia zaidi klabu yao ya Athletic Kluba Bilbao au ukipenda unaweza kutamka Bilboko Athletic Kluba, wewe zaidi unaijua kama Athletic Bilbao.

Wakazi wa miji ya Hispania, wengi wana utamaduni wa kujivunia timu za miji yao. Si rahisi mtu wa Madrid akaisifia Derpotivo la Coruna, kila mmoja ana uzalendo na mkoa wake, pia wanasaidiwa na suala la kutokuwa na makabila au kuingia katika suala la timu. Mfano, unamkuta Mhaya amechanganyikiwa, ashangilie ipi, zinapokutana Yanga na Kagera Sugar!


Unaishi Bilbao, timu yake ni Bilbao, maisha yako ni Barcelona, unaweza kuchagua kati ya timu za mji huo, FC Barcelona au Espanyol.    
Bilbao imewahi kuwa na mafanikio huko nyuma, lakini kipindi kilichobaki ni klabu inayoonyesha mapenzi ya kuwapa mashabiki wa eneo lake burudani ya La Liga.

Wachezaji nyota kama Lionel Messi, Luis Suarez, Cristano Ronaldo, Gareth Bale husafiri na timu zao maarufu kuwafuata mashabiki wa timu hiyo kwa kuwa timu yao ipo kwenye ligi.

  
Mashabiki wanajua bila hivyo, mastaa hao wasingekuwa na sababu ya kuja hapo, hivyo wanachofanya ni kuiunga mkono timu yao kwa asilimia mia, ikiwa ni pamoja na kununua vifaa pia kwenda uwanjanim kwa wingi sana.

Daniel Munez, anasema asili yake ni nchini Colombia. Lakini ameishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 38 na mapenzi ya Bilbao na mashabiki wake ni makubwa kuliko ya mke na mume.

“Hakuna asiyeipenda timu hapa, wachezaji wanaishi kama familia na mashabiki. Wakati mwingine, mashabiki huwaalika wachezaji nyumbani kwa kwa chakula. Siku ikifungwa timu, unakuwa umefungwa mji mzima. Wakishinda, basi ni sherehe utafikiri ni siku ya uhuru,” anasema Munez katika mahojiano na Championi Jumatano mjini hapa.

            
Atletic Bilbao si tajiri, lakini ndiyo timu pekee kwenye La Liga inafanana kabisa na vigogo wakubwa yaani Real Madrid na FC Barcelona.
Inafanana na timu hizo kwa mambo mawili, kwanza tokea kuanza kwa La Liga msimu wa 1928-29, haijawahi kuteremka daraja hadi sasa. Timu zote zimekuwa zikipanda na kushuka wakiwemo vigogo Valencia, Atletico Madrid, Sevilla, Derpotivo La Coruna na wengine.

Atletic Bilbao, Real Madrid na Barcelona ndiyo timu ambazo hazijawahi kuteremka daraja hata mara moja na zinaendelea kudumu.

Kingine ambacho inafanana na Real Madrid na FC Barcelona. Atletic Bilbao ni timu ya tatu kati ya 20 za La Liga inayomilikiwa na wanachama, nyingine ni hizo mbili kubwa. Zilizobaki ni mali ya makampuni mbalimbali.

Pamoja na Atletic Bilbao kuwa timu ambayo ni mali ya wanachama na haijawahi kuteremka daraja kutoka La Liga. Kweli inazidiwa fedha na wakubwa hao Real Madrid na FC Barcelona, lakini nayo ina jambo ambalo hakuna timu nyingine inafanya katika La Liga na Hispania yote ikiwezekana.

Tokea mwaka 1928 ilipoingia La Liga, Atletic Bilbao haijawahi kusajili mchezaji wan je ya eneo lao la Bilbao. Wote wanaocheza katika kikosi hicho ni wale waliokulia katika eneo hilo. Yenyewe zaidi hufaidika na kuuza, au wanaobaki wanaitumikia klabu hiyo kwa juhudi kuu, siku wakistaafu wanaangwa kwa heshima kubwa.


Roberto Garcia, mmoja wa wanaohusika na masuala ua uipangaji wa mipango ya kila msimu na kusimamia uendeshaji wa kikosi cha Atletic Bilbao anasema kamwe hawawezi kubadilisha mambo na mfumo huo, huenda ukaendelea milele.

“Kuna faida nyingi zaidi kwa maana ya maisha katika eneo letu. Vijana wa hapa (Bilbao), wamekuwa wakijituma kwa juhudi wakijua kuna nafasi.

  

“Mfano kuna kijana ameonekana ana nafasi na klabu kubwa kama Madrid ikamhitaji, tunamuuza. Lakini tutamfuatilia kwa karibu kujua anaendaje, siku wakisema wanamuacha tutamchukua tena. Klabu kubwa zina mambo mengi sana, wachezaji wengi wanashindwa.

“Lakini wachezaji wa hapa nyumbani, wameendelea kuwa msaada na tunaamini ni mpangilio sahihi, maana timu haijawahi kuteremka daraja.
 

"Hili ni jambo la kihistoria kwetu, tunataka kulidumisha. Ingawa tunatamani kupata makombe, lakini tukikosa sawa tu lakini tusiteremke daraja.

“Mapendi ya wananchi wa eneo hili na klabu ni makubwa sana. Wako walianza kushangilia timu wakati wanafunzi wanasoma. Leo wana wajukuu na wanaendelea kushangilia na kuhamasisha. Hivyo utamaduni huu utabaki kwa miaka mingi ijayo,” anasema Garcia.

Garcia anasema hawaamini kuwa familia za eneo hilo zinahitaji msaada wa uzalishaji wa watoto wenye vipaji kwa kuwa waliopo tayari wamezaa watoto walioendeleza utamaduni huo miaka nenda rudi, wana makocha wamefanya utamaduni udumu miaka yote na wengine wanakuzwa.
 

WATU WA ATLETICO BILBAO
Wanaamini mapenzi ya dhati kwenye ukuzaji wa watu. Hata katika maisha ya kawaida, wao ni watu wanaopeana nafasi.

Wanaamini mtu asiyetaka kukuza watu kwa kile anachokijua, anapaswa kuitwa shetani na asiyetaka kutoa nafasi kwa wenzake, hastahili kuishi kwenye dunia ya sasa.
Makombe waliyowahi kuyatwaa na miaka:


La Liga (8): 1929–30, 1930–31, 1933–34, 1935–36, 1942–43, 1955–56, 1982–83, 1983–84


Copa del Rey (23): 1903, 1904, 1910, 1911, 1914, 1915, 1916, 1921, 1923, 1930, 1931, 1932, 1933, 1943, 1944, 1944–45, 1949–50, 1955, 1956, 1958, 1969, 1972–73, 1983–84.

Supercopa de EspaƱa (2): 1984, 2015
Copa Eva Duarte (1): 1950

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV