August 31, 2016

MAVUGO KAZINI
Straika wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, hivi karibuni alionekana kama amelijaribu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kuvaa jezi zenye namba mbili tofauti kwenye Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu uliofanyika Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Mavugo alivunja kanuni ya shirikisho hilo baada ya kuvaa jezi namba 11.

Hii ilikuwa namba tofauti na ile ambayo aliivaa kwenye mchezo dhidi ya Ndanda ambapo alivaa namba 9 ambayo ilisajiliwa kihalali kuwa ni namba yake.

Kutokana na hali hiyo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Boniface Wambura, aliliambia Championi Jumatano kuwa, kitendo hicho cha Mavugo kuvaa jezi zenye namba mbili tofauti katika mechi mbili tofauti za ligi hiyo ni kosa kubwa, hivyo wanamchunguza na anaweza kuchukuliwa hatua.

“Mchezaji mmoja kutumia namba mbili tofauti katika ligi ni kosa kikanuni, hivyo kama Mavugo amefanya hivyo, basi atakuwa amevunja kanuni hiyo.

“Hata hivyo, kwa sasa siwezi kulizungumzia sana suala hilo kwa sababu bado halijanifikia mezani kwangu,” alisema Wambura kwa ufupi huku pia akisita kuweka wazi adhabu ambayo Mavugo anaweza kukumbana nayo baada ya kutenda kosa hilo.

Alipoulizwa Mavugo kuhusiana na suala hilo alisema: “ Binafsi sikujua kama ni kosa lakini ninachoweza kusema ni kwamba niliamua kuitumia jezi namba 11 na kuachana na namba 9 kwa sababu nilikuwa nikiipenda.


“Lakini pia imeachwa na mtu ambaye mashabiki wengi wa Simba walikuwa wakimpenda sana, hivyo na mimi kwa kuvaa jezi hiyo naamini nitawafanya mashabiki wa timu yangu kuwa karibu na mimi zaidi.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV