August 31, 2016



Baada ya Yanga kufanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa kuifunga African Lyon mabao 3-0 kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, winga hatari wa timu hiyo, Simon Msuva ameibuka na kuweka wazi juu ya mipango ya ubingwa ya timu hiyo msimu huu.

Msuva aliyecheza kwa kiwango cha juu na kufunga bao la pili katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar ameeleza pia kuhusiana na ndoto zake za kuibuka mfungaji bora msimu huu kama alivyofanya msimu wa 2014/15.

Winga huyo amefafanua kuwa, ingawa wameanza kwa ushindi mzuri msimu huu lakini bado wanahitaji kujiangalia walipofika na kuitathmini ligi itakavyokuwa baada ya mechi sita zaidi ambazo ni sawa na dakika 540, kisha baada ya hapo watajua kama wana njia nyepesi kutwaa ubingwa au la.

“Nia yetu ni kufanya vizuri msimu huu, lakini kwa sasa ni mapema kuzungumzia hilo, ndiyo kwanza mechi yetu ya kwanza ila imekuwa vizuri tumeibuka na ushindi mzuri. Kwa jinsi mambo yalivyo, ishu ya uelekeo wa ubingwa itabainika baada ya mechi sita mbele.

“Lyon ndiyo kwanza imepanda daraja, lakini hatukuliangalia hilo wala kuweka dharau, cha msingi ilikuwa tupambane na kutengeneza mazingira mapema, ndiyo ilikuwa siri kubwa ya kuibuka na ushindi wa kwanza mnono,” alisema Msuva.

Kwa kauli ya kutazama mwelekeo wa Yanga baada ya mechi sita, Msuva alimaanisha kuuvuka mtihani wa mechi sita zilizo mbele yao ambapo itaanza ugenini kucheza na Ndanda FC, kisha itacheza na Majimaji, Mwadui FC,  Stand United, baada ya hapo itaumana na mahasimu wao, Simba SC na mechi ya sita itakuwa kati ya Ruvu Shooting ambayo haijapangiwa tarehe au Mtibwa Sugar. Ukipiga kwa hesabu za muda, maana yake ni dakika 540, kwani kila mechi ina dakika 90.

Hata hivyo, kuhusiana na ufungaji bora, Msuva pia alieleza: “Dah! Siwezi kusema kitu kwa sasa, kama nilivyoeleza huu ni mwanzo na sijajua mbele itakuwaje, kinachotakiwa ni kuzidi kujipanga zaidi, maana ndiyo kwanza vita imeanza.”

Msuva aliwahi kuibuka mfungaji bora wa msimu wa 2014/15, kwa kutupia mabao 17, msimu uliopita hakufanikiwa kutetea kiatu chake hicho ambacho kilitua kwa mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe aliyefunga mara 21 huku mwenyewe akifunga mabao tisa tu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic