September 2, 2016Na Saleh Ally
NAMSHUKURU Mwenyezi Mungu kwa kuwa hili nililiona mapema na kulizungumzia nikitumia kurasa mbili kupinga mgogoro wa Klabu ya Stand United ambao ulikuwa wazi kwa kila kitu kwamba kuna kundi linaonewa na kila mmoja anajua.

Uongozi wa wale makondakta au wapiga debe kutaka kupokonywa timu na wale ambao ilielezwa kwamba wanaungwa mkono na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilikuwa siyo jambo zuri.

Ilionekana wazi kwamba uongozi wa Stand United, ulihangaika na timu hiyo tangu ilipoanzishwa. Baada ya hapo wakafanikiwa kupata udhamini huo mnono uliowawezesha kupata hadi Sh bilioni 1.2 kwa mwaka, ambao unawafanya wao kuwa na mkataba mnono wa udhamini kuliko hata walionao Yanga au Simba. Swali, hawa waliokuwa wakiidai Stand United sasa, wako wapi?

Nilieleza hofu ya kuwatisha wadhamini. Nilieleza namna mgogoro ulivyoibuka mara baada ya udhamini mnono. Kuna watu walikuwa madalali, baada ya kuona fedha ni nyingi eti wakaona wale makondakta hawawezi tena kuiongoza timu, kisa fedha ni nyingi.

TFF inaingia kwenye shutuma, kwa kuwa kila kitu kipo wazi. Watu wote wanajua hawa ndiyo walikuwa viongozi wa Stand, waanzilishi wa timu hiyo ndiyo maana nikasema TFF inatengeneza hofu kwamba wananchi wenye kiwango au kipato cha chini kama wakianzisha timu, kwenye shida wanahangaika nayo, ikikua au kupata udhamini inatakiwa wapewe walio wasomi au wale wanaojua mahesabu, hiki ni kituko.

Sasa wadhamini wakuu wa Stand, Kampuni ya Acacia wameamua kujitokea na wazi kabisa tatizo ni hiyo migogoro. Hiki ni kitu kibaya kabisa ambacho kimetokea kipindi ambacho TFF ya Jamal Malinzi ikiwa madarakani na imeshindwa kulitatua jambo hilo kwa kuwa ilitengeneza upande.

Ingekuwa vema kabisa kama TFF ingelimaliza kwa haki kwa kuwa hakukuwa na asiyejua viongozi halali wa Stand. Sasa mgogoro unairudisha Stand United katika maisha ya enzi za makondakta. Kitu ambacho hata waliong’ang’ania huenda wakaenda nayo muda mfupi wakianza kwa kujitutumua. Unajua, ukitegemea kuchuma, halafu baadaye kukawa hakuna cha kuchuma hali huwa mbaya zaidi.

Shinyanga ni kati ya mikoa yenye vipaji vingi vya wanasoka. Lakini imekuwa ikishindwa kuendelea kwa kuwa viongozi wake wa soka wa mkoa ni watu wabinafsi ambao wanaona kuangalia suala la maslahi binafsi ndiyo jema.

Miaka nenda rudi baada ya biashara iliyoitwa Shinyanga Shooting baadaye kuteremka daraja, hakuna timu iliyouwakilisha mkoa huo katika ligi kuu hadi wapiga debe wa stendi ya mkoa walipoanzisha timu na mwisho kujichangisha kwa kipato chao kidogo kuisaidia kufika ilipo sasa.

Wamepata udhamini, inaonekana hawana uwezo wa kuendeleza walipofikia. Badala yake watu fulani ndiyo wanaweza na huenda hata serikali ikaelezwa mambo ambayo si sawa kwa kuwa wahusika wanahitaji kuhalalisha uozo wao.

Acacia wanajua walikuwa wanafanya kazi na yupi kwa kuwa hata kabla ya kudhamini, walikuwa wakisaidiana na Stand United, walipovutiwa nao, wakaona kuingia na kuwa wadhamini rasmi badala ya wafadhili.

Maana yake hivi; hadi wanafikia kujitoa, hata wao Acacia wameiona kasoro na wanajua kuna tatizo kwa kuwa wanaelewa mwendo wa Stand United hata kabla haijapanda daraja hadi Ligi Kuu Bara.

Tamaa na uzandiki wa viongozi wa soka nchini imekuwa sumu kubwa ya maendeleo ya soka. Leo kwa mara nyingine, imeonyesha tamaa hiyo ni adui maana inaondoa moja ya udhamini bora kabisa katika klabu za soka nchini kwa tamaa ya wachache ambalo ni jambo baya na waliosababisha ni watu wanaopaswa kulaaniwa kwa nguvu zote.

Hii ni aibu, hii ni hatari kwa afya ya kutengeneza imani ya mchezo wa soka kwamba unahitaji wadhamini. Maana kila wanapojitokeza na kuweka fedha tu, mafundi wa kuzila wanajitokeza na kusababisha tatizo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV