October 3, 2016



Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ametoka kifua mbele akisema hana wasiwasi kuhusu suala la kuzidiwa pointi nyingi na Simba SC huku akitaja moja ya vinavyompa jeuri hiyo ni mechi za mikoani ambazo Simba hajacheza hata moja mpaka sasa.

Baada ya mechi yao ya wiki iliyopita waliyomaliza kwa sare ya 1-1, Simba imeendelea kusalia kileleni kwa pointi 17, ikishinda mechi tano na sare mbili. 

Pluijm ambaye kikosi chake kina pointi 11, ameeleza kuwa kuzidiwa pointi ni moja ya hali ya ushindani kwenye ligi na kwamba bado kuna mechi nyingi mbele yao, hivyo uwanja wa mashindano bado mpana, hasa ukizingatia kuwa Simba imevuna pointi nyingi ikiwa nyumbani na bado haijatoka mikoani ambako kuna shughuli nzito.

“Kweli tumezidiwa pointi sita lakini hii ni ligi na ina mechi nyingi, bado uwanja ni mpana, ukiangalia wao wamevuna pointi nyingi kwa kushinda wakiwa uwanja wa nyumbani, hawajatoka kupambana ugenini hata mechi moja.

“Nafikiri baada ya kucheza mechi kadhaa ugenini na kupata matokeo ndiyo tutapima vizuri kuhusiana na pengo walilotuacha wakiwa kileleni. Kitaalamu huwezi kuwa na uhakika kuwa utapoteza ukiwa ugenini lakini kiuhalisia inafahamika kuwa ukiwa ugenini inakuwaje,” alisema Pluijm.

Pamoja na hayo, lakini mashabiki wa Yanga pia wamekuwa wakitambia mechi yao ya kiporo dhidi ya JKT Ruvu kuwa mechi hiyo ni uhakika kuvuna pointi tatu na kuikaribia Simba kileleni.


Katika mechi sita za Yanga mpaka sasa, tatu imecheza ikiwa nyumbani na kufanikiwa kuzifunga African Lyon mabao 3-0, Majimaji 3-0 na sare ya 1-1 dhidi ya Simba. Ikiwa ugenini dhidi ya Ndanda ilipata sare ya 0-0, ilipocheza na Mwadui ikashinda 2-0 kabla ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Stand United.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic