October 3, 2016


Huku Simba ikiingia kwenye maandalizi ya mchezo wao mgumu unaofuata dhidi ya Prisons, italazimika kuikosa huduma ya kocha wake msaidizi, Mganda, Jackson Mayanja ambaye jana alitarajia kurejea kwao, Kampala.

Mayanja ambaye amesaidiana na bosi wake, Mcameroon, Joseph Omog kuiongoza Simba kushinda michezo mitano na kusuluhu miwili, ikiwa kileleni kwa pointi 17, amekwenda kwao kutokana na matatizo ya kifamilia.

Mayanja amesema kuwa atakosekana katika siku za mwanzoni mwa maandalizi ya mechi na Prisons kwa ajili ya kwenda kutoa pole na kuzungumza na familia yake baada ya kufiwa na mdogo wake, Ronald Galabuzi.

Simba imepangwa kucheza na Prisons, Oktoba 8, halafu Oktoba 12 itavaana na Mbeya City.

“Timu kwa sasa imepumzika mpaka Jumanne (kesho) kwa hiyo naona huu ndiyo muda sahihi na mimi niende japo nyumbani kidogo maana sikwenda wakati wa msiba, kwa hiyo bora niende nikatoe hata pole, nizungumze na familia kidogo.


“Msiba huu ndiyo ule uliotokea kama wiki mbili zilizopita. Sitakaa sana najua kuna mchezo mbele dhidi ya Prisons na Mbeya City, kwa hiyo itachukua kama siku mbili au tatu kisha nitarejea hapa kuendelea na majukumu ya timu,” alisema Mayanja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV