October 21, 2016



Na Saleh Ally
MARA kadhaa, nimewahi kumzungumzia kinda Farid Mussa, kwamba ni kati ya nyota ambao Tanzania imewapata na anapaswa kutupiwa jicho.

Nilieleza kuwa sina hofu hata kidogo na Farid kupiga hatua hadi kucheza Ulaya. Tena nikasisitiza muda wake ni sasa kwa kuwa wachezaji wengi kutoka hapa nyumbani wamefeli kutokana na umri na wengi hukumbuka kwenda kucheza nje, umri ukiwa umewatupa mkono.

Klabu ya Azam ilifanya juhudi na kufanikiwa kumpeleka Hispania kwa ajili ya majaribio, akafanikiwa, yaani amefuzu.

Sasa ni zaidi ya miezi miwili, kijana huyo hajui la kufanya kwa kuwa Uhamisho wake wa Kimataifa (ITC) umetumwa Hispania katika klabu ya Daraja la Kwanza ya Tenerife, lakini hawezi kuichezea kwa kuwa tumeelezwa tatizo ni visa.

Azam FC imeeleza kwamba ishu ya Farid imekwama kwa kuwa hajapewa visa, hivyo kuomba asaidiwe lakini mimi nilianza kuingia hofu mapema kwamba kuna tatizo ndani ya suala hilo. Nikiwa Hispania katika mambo yangu, niliamua kufunga safari hadi Tenerife hata bila ya kuwa na mwenyeji.

Nilifanikiwa kuiona Tenerife ikicheza mechi moja ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1. Nilivyowaona wachezaji wenzake na Farid, hakika sikuwa na hofu hata kidogo kuwa wakimpa nafasi atafanya vizuri na hakuna wa kumzuia hata chembe.

Nikaanza kufanya uchunguzi kutaka kujua ni kwa nini Farid anaendelea kubaki Dar es Salaam. Kulikuwa na ugumu kwa kuwa viongozi walionekana kuwa na hofu kunijibu na hakika ilionekana suala lenyewe, ndani yake kama kuna figisu hivi.

Mmoja wa viongozi anayeshughulikia masuala ya soka katika eneo la Tenerife, alinieleza kuwa Farid ana tatizo la ndani ya Tenerife. Kwamba kuna mgogoro ambao unafanya akwame kwenda na inaonekana katikati katika usajili wake, kulikosekana uaminifu.

Hakutaka kufafanua zaidi kuhusiana na uaminifu huo. Nilianza kupata harufu ya shida na ndiyo maana mchezaji huyo anaendelea kubaki nje ya uwanja.

Niliporejea hapa, niligundua Farid alichoka na kuacha mazoezi na Azam FC, akaamua kwenda Morogoro kwa masuala yake ya kifamilia. Jambo jingine ambalo niliona halikuwa sahihi kwake.

Kweli kachoka kufanya tu mazoezi bila ya kucheza mechi za mashindano, si jambo zuri kwa mchezaji yeyote yule anayetaka maendeleo, ni hatari zaidi kwa mchezaji kukaa nje bila ya mazoezi kabisa hasa chini ya wasimamizi wanaofanya mambo kitaalamu.

Ninajua ndani ya suala hilo kutakuwa na figisu, namna wale viongozi wa Tenerife walivyokwepa kulizungumzia, hakuna shaka ndani yake kuna shida ambayo wanapaswa kuifanyia kazi.

Huenda Tenerife wanaweza wasiwe na shida sana, lakini Azam FC wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuepuka kumpoteza Farid kwani si wao peke yao, ni kijana wa taifa zima.

Farid ni hazina ya taifa, kama kuna jambo kati ya Tenerife na Azam FC, au kuna kitu kimesababisha hali ya kutoelewana, basi kifanyiwe kazi na Farid arejee uwanjani na kuendelea kupambana. Kwani hata akikosa Tenerife, bado ana nafasi ya kuendelea zaidi na kucheza kwingineko Ulaya.

Lazima tukubali, Tanzania inahitaji wachezaji wengi kucheza nje ya Afrika na hasa Ulaya ili kuwa na mabadiliko kwenye timu ya taifa. Farid anaweza kuwa sehemu ya mabadiliko kama ataendelea kucheza.

Kuendelea kubaki nje ya uwanja kama ilivyo sasa, tena saikolojia yake ikiendelea kuathirika na mbaya zaidi kama hakuna anayekaa karibu naye. Mwisho atakata tamaa na kudondoka katika mbio za mapambano kukimbilia mafanikio.

 Kinda huyu kuendelea kukaa nje, si sawa hata kidogo. Suala hilo Azam FC wanapaswa kuliangalia kwa upana wa utaifa na maendeleo ya kinda huyo.

Vizuri iwe sasa kabla hajakata tamaa, inawezekana kweli Azam FC wana mambo yao mengi muhimu ya kufanya, lakini Farid wanaweza kumuweka sehemu ya mambo muhimu na kulimaliza suala lake ili wamsaidie aendelee. Tafadhali, asipotee wakati uwezo wa kumuendeleza upo. Kuacha aishe au amalizike, ni kujimaliza wenyewe.



2 COMMENTS:

  1. Hujui tatizo hasa ni nini, na mhusika hasa ni nani, lkn unawalaumu AZAM kuwa wanamchimbia shimoni. Acha kukurupuka, si lazima uandike kila jambo.

    ReplyDelete
  2. Hujui tatizo hasa ni nini, na mhusika hasa ni nani, lkn unawalaumu AZAM kuwa wanamchimbia shimoni. Acha kukurupuka, si lazima uandike kila jambo.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic