October 15, 2016


Maneno yameanza kwani siku chache baada ya Obrey Chirwa kufunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu Bara, akiichezea Yanga, kocha wake Hans van Der Pluijm ametupa kijembe.

Pluijm, raia wa Uholanzi, ametupa kijembe hicho kwa waliokuwa wakibeza uwezo wa kufunga wa Chirwa, mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka FC Platinum ya Zimbabwe.

Chirwa, raia wa Zambia, tangu ajiunge na Yanga msimu huu hakufanikiwa kufunga bao kwenye michezo ya kirafiki, ligi hata ile michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Jumatano wiki hii kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Chirwa alifunga bao lake la kwanza katika ligi dhidi ya Mtibwa Sugar na kuiwezesha Yanga kushinda mabao 3-1.

Chirwa alifunga bao hilo dakika ya 45 baada ya kupokea pasi ya Simon Msuva ambaye ametimiza mabao 50 na kuifungia Yanga la kwanza katika mchezo huo. Wafungaji wengine ni Msuva na Donald Ngoma.

Pluijm alisema: “Siku zote mchezaji anapokuwa mpya, mashabiki wote wanamuangalia yeye wakisubiria kuona kitu kipya kutoka kwake.

“Mashabiki wasipoona kitu kipya kutoka kwake, basi ni lazima waanze kubeza kiwango chake, bao hili alilofunga Chirwa limezima yote yaliyokuwa yanasemwa dhidi yake.


“Ninaamini bao lile litampa hali ya kujiamini na kucheza bila ya presha ya mashabiki aliyokuwa anaipata, huu ndiyo mwanzo mzuri wa Chirwa kuendelea kufunga mabao kwenye mechi zetu za ligi kuu.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV