October 19, 2016

TAMBWE
Kasi ya kuzifumania nyavu ya winga wa Simba, Shiza Kichuya aliyonayo sasa katika Ligi Kuu Bara, imempagawisha mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe ambaye amekiri kuwa jamaa anatisha.

Tambwe amedai kuwa kwa Kichuya yupo vizuri lakini anatakiwa kuwa makini kuhakikisha analinda kiwango chake hicho kwa kuzingatia misingi na maadili ya soka.

Hivi sasa Kichuya ndiye gumzo la mtaa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzifumania nyavu ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani tangu alipojiunga na Simba akitokea Mtibwa Sugar.

KICHUYA
Kichuya anayetumia mguu wa kushoto, ndiye anayeongoza kwa kuzifumania nyavu katika ligi hiyo akiwa na mabao saba aliyoyafunga kwenye mechi tisa alizoitumikia Simba mpaka sasa, nafasi ya pili inashikiliwa na Omary Mponda wa Ndanda FC akiwa na mabao matano wakati  Tambwe ambaye msimu uliopita ndiye aliyekuwa mfungaji bora anashika nafasi ya tatu akiwa na mabao manne.

Tambwe alisema Kichuya yupo vizuri na ni msaada mkubwa kwa timu yake ya Simba hivyo kama hatabadilika anaamini anaweza kufanya maajabu msimu huu.

 “Asibweteke na sifa kwa mafanikio hayo machache aliyoyapata hivi sasa kama anataka kudumu.
“Kazi anayoifanya uwanjani ninaona, yupo vizuri kwa sasa kama ataongeza juhudi zaidi mazoezini na kuzingatia miiko na maadili ya soka atapata mafanikio zaidi.


“Kuhusu kuibuka mfungaji bora msimu huu hilo siwezi kutabiri kwa sababu ligi bado mbichi na kuna wachezaji wengi ambao wanafanya vizuri kama yeye lakini ukweli ni mchezaji hatari,” alisema Tambwe ambaye ni shabiki mkubwa wa Liverpool na Barcelona.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV