October 15, 2016Na Saleh Ally
KARIBU kila sehemu unapozungumziwa mchezo wa soka na hasa Ligi Kuu Bara, gumzo zaidi ni kiungo mshambulizi wa Simba, Shiza Kichuya.
Kichuya ametokea Mtibwa Sugar na kujiunga na Simba, lakini sasa amekuwa tegemeo kubwa kuanzia katika kikosi cha Simba, pia tumaini kwa mashabiki.

Mashabiki wa Simba wana furaha ya kikosi chao kuwa bora kwa maana ya muunganiko wa timu. Lakini unapozungumzia Kichuya, ni sehemu ya ufunguo wa wao kutaka wanachotaka.

Kichuya ameanza kuonyesha tofauti kubwa sana na wachezaji wengi wazawa. Kwangu ninaona, Simon Msuva wa Yanga amekuwa sehemu ya mfano, ingawa amekuwa hana bahati kuu kutoka kwa mashabiki wa Yanga, wanampenda wakati wa raha tu, akishuka kiwango au mpira ‘kumkataa’, wote wanageuka.

Lakini Msuva hajawahi kukata tamaa, kila mechi utamuona ni mchezaji anayetaka kushinda au kufanikiwa. Ni mchezaji anayetaka kupata au kuona mafanikio.

Utamjua aliye tofauti, mfano anavyokimbia, anavyosimama, anavyoupokea mpira na kadhalika. ‘Body language’ au mwenendo wa mwili, unaeleza mengi kama ukiwa mtulivu wakati unaangalia.

Kichuya alionyesha wazi ameamua kwenda Simba, hakuwa na muda wa kupoteza au kuyumba. Aliwaonyesha Mtibwa Sugar kwamba yeye anataka kwenda Simba na akasisitiza mwisho akatua Simba.

Alionyesha alitaka kufika Simba na kufanya anachotaka. Anaonyesha anataka kufanya kweli lakini ana mambo ambayo yanaweza kuwa somo kwa wachezaji wengine wa nyumbani.


Hatabiriki:
Kwanza, ni mchezaji ambaye hana tamaa ya kufunga kwa kuwakwamisha wengine, utaona kwake inakuwa rahisi zaidi kufanikiwa. Kichuya yuko tayari kutoa pasi kwa wengine wafunge, ndiyo maana inakuwa rahisi kwake pia kufunga.

Katika mpira, kutoa pasi ni sehemu ya chenga bora kabisa, nitakueleza. Mchezaji anayetoa pasi anakuwa na uwezo wa juu zaidi katika suala la kutotabirika. Kwani mlinzi anapokutana naye, anakuwa anashindwa kutabiri lengo lake hasa ni lipi. Lakini kwa mchoyo hadi anajulikana, inakuwa rahisi zaidi kumdhibiti.

Kichuya ni mgumu kumdhibiti, kwa kuwa anaweza akafanya kitu chochote, wakati wowote tena bila ya kutegemewa atafanya nini.


Kujiamini:
Pamoja na kuwa na umbo dogo, Kichuya anajiamini sana. Ni mtulivu katika kila jambo analolifanya uwanjani kwa kuwa amekuwa akitaka kufanya kwa uhakika.

Wachezaji wengi wazawa, hawajiamini, waoga katika utekelezaji wa wanayopanga na hali hiyo huzaa papara kwao na wao kushindwa kufanya mambo kwa ubora wa juu. Kichuya anaweza kuwa somo kwao na kuwasaidia kusonga kwa uhakika zaidi.

Kujituma:
Ukimuona Kichuya akiwa uwanjani, ni rahisi sana kumtofautisha na wachezaji wengi wa nyumbani.

Utamuona ni mwenye kasi, anayepambana kwa juhudi na ule mwonekano wa mtu anayetaka kushinda unaonekana waziwazi.

Hii inaweza kuwa rahisi sana kuiona kwa wachezaji wa nje, mfano Lionel Messi au Cristiano Ronaldo ni wachezaji wanaokuonyesha wanataka kitu fulani na wanataka kweli kwa juhudi kuu wanayokuwa nayo.

Hofu:
Kichuya ameishinda hofu ambayo imewatafuna wachezaji wengi wazalendo ambao wana uwezo mkubwa lakini wameshindwa kujipambanua na kuyashinda mazoea.

Wadau wengi wa soka wanaamini wachezaji kutoka nje ndiyo bora zaidi. Kichuya amesema hapana, hata yeye anaweza, iwe kwa kutoa pasi, kufunga au kuisaidia timu kwa kukaba.

Wachezaji wengi wazawa wana uwezo kama wa Kichuya. Lakini hawajawa tayari kwa kuwa hawaaminiki. Wote tunajua miezi miwili tu iliyopita, Kichuya hakuwa akiaminika Simba, lakini sasa utawaeleza nini!

Juma Mahadhi ambaye yuko Yanga, bado hajaonyesha kama anaweza kujiamini na akafanya anachoona sahihi. Lakini ninaamini ana uwezo mkubwa kabisa na alitakiwa kuwa gumzo kama Kichuya sasa au ikiwezekana zaidi.

Wachezaji wengi wazawa ni waoga, huenda kwa kuwa bado wanaamini kufika Yanga na Simba ni mwisho wa safari, hivyo bora kujificha kwenye mwamvuli. Pia wanaogopa sana kukosea huku wakiwa wamesahau, hakuna mafanikio na hasa katika kukua kama haukosei.

Wanaokosea ndiyo wenye nafasi ya kukua zaidi. Kosea ujifunze, ujirekebishe na baadaye ubadilike na hapo utakua. Wazawa acheni woga na kufanya mambo kwa mazoea.

Lengo si kumsifia sana Kichuya, lengo ni kusema hali halisi na mambo yalivyo. Lakini vizuri pia kuweka msisitizo. Ndani ya mechi nane, tayari Kichuya amefikisha mabao sita, hii si kazi ndogo lakini kazi yake haijaisha.

Haya nimeyasema ni machache niliyoyaona kwake. Lakini anaweza asionekane lolote kama atashindwa kufanya mwendelezo na pia kufeli, hii itaonyesha hata yeye alikuwa aliyechangamka mwanzo na mwisho akalewa sifa.

Sifa mbaya zaidi ya wachezaji wengi wazawa ni kuleta sifa. Angalia Amissi Tambwe, anajua kazi yake ni kufunga, hachoki kufunga hata iweje na hajalewa sifa ndiyo maana anaonekana ni hatari na hatari yake ni ya muda mrefu.

Lakini hatari ya wazawa ni ya kubahatisha au muda mrefu. Hivyo Kichuya kama ameamua kukimbia kweli, asijisahau akapumzika maana wengine watapita na kumuacha alipo. Kulewa sifa, kujisahau kwa ajili ya starehe kwa kuwa ni maarufu ni sehemu ya sumu. Badala yake anapaswa kuamini ndiyo anaanza, safari bado ndefu na lazima abaki kuwa binadamu badala ya asiyeshikika.


MSIMAMO BARA
                             P      W     D      L      F      A      GD  PTS
1      Simba          8      6      2      0      15    3      12    20  
2      Stand           9      5      4      0      9      3      6      19  
3      Kagera         9      4      3      2      6      4      2      15  
4      Yanga          7      4      2      1      12    3      9      14  
5      Mtibwa       9      4      2      3      9      9      0      14  
       


MSIMAMO WA WAFUNGAJI
Shiza Kichuya                  Simba      6
Omary Mponda               Ndanda   5
Amissi Tambwe              Yanga      4
Abrahman Mussa           Ruvu        4
John Bocco                Azam       3
Raphael Daud                  Mbeya     3
Laudit Mavugo                Simba      3
Hood Mayanja                 Lyon        3
Rashid Mandawa            Mtibwa   3
Venance Ludovick          Mbao       3
Ibrahim Ajib                         Simba      3
Haruna Chanongo          Mtibwa   3
Deus Kaseke                        Yanga      2
Wazir Junior                   Toto         2
Samwel Kamuntu                  JKT           2
Jamal Mnyate                      Simba      2
Adam Kingwande                Stand       2
Hamis Mcha                   Azam       2
Shaaban Kisiga                     Ruvu        2
Simon Msuva                 Yanga      2
Pastory Athanas              Stand       2
Danny Mrwanda             Kagera     2
Paul Nonga                           Mwadui  2
Donald Ngoma                Yanga      2
Boniface Maganga          Mbao       2
Ally Nassoro            Kagera     20 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV