October 19, 2016


Winga machachari na tegemeo Yanga, Simon Msuva, amemtabiria ufungaji bora kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya huku akimtahadharisha kuhusu Mrundi, Amissi Tambwe.

Kauli hiyo, ameitoa ikiwa ni siku chache baada ya mashabiki wa Simba kumtabiria ufungaji bora kiungo huyo kutokana na kasi yake kubwa aliyoanza nayo ya kufunga mabao.

Kichuya aliyetua kuichezea Simba msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Mtibwa Sugar, hadi hivi sasa anaongoza kwenye ufungaji akifunga mabao saba, Omari Mponda wa Ndanda FC (matano) na Tambwe akipachika manne.

Msuva alisema kiungo huyo ana uwezo wa kutwaa ufungaji bora kama akihitaji, licha ya kuwa ni mapema kutabiri ufungaji kutokana na ushindani mkubwa wa timu msimu huu.

Amesema, wakati kiungo huyo akipewa nafasi ya ufungaji bora msimu huu, basi waangaliwe na wachezaji wengine hatari wenye rekodi, akiwemo Tambwe.

“Kichuya ni mchezaji mzuri na mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao na anayeweza kuchukua ufungaji bora msimu huu kama kweli akihitaji kufanya hivyo.

“Lakini anatakiwa apambane siyo kidogo, kwani wapo washambuliaji wengi hatari wenye uchu wa kufunga mabao kama vile Tambwe ambaye hatabiriki kutokana na aina yake ya uchezaji akiwa uwanjani.

“Mimi binafsi namuombea kwa Mungu atimize ndoto zake, lakini ajipange kwa sababu ligi kuu yenyewe ndiyo kwanza mbichi kama sisi Yanga tumecheza mechi saba, hivyo ni ngumu kutabiri ubingwa na hata ufungaji bora,” alisema Msuva aliyewahi kuwa mfungaji bora msimu wa 2014/2015, huku Tambwe akichukua misimu miwili 2013/2014 na 2015/2016.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV