October 19, 2016


VICENT
Kipa wa Simba, Vincent Angban mpaka sasa ndiye aliyecheza mechi nyingi bila kuruhusu bao ‘clean sheet’, akifanya hivyo kwenye michezo sita kati ya tisa iliyocheza Simba huku akisimama golini mechi zote, sawa na dakika 810.

Muivory Coast huyo aliyetoswa na Azam majaribioni mwanzoni mwa msimu kwa kile walichosema kiwango chake ni hafifu, mpaka sasa amefanikiwa kuiweka Simba kileleni mwa msimamo, huku akiwa ameruhusu mabao matatu tu katika mechi tatu pekee.

Simba inaungana na Yanga ambayo pia imeruhusu idadi hiyo ya mabao, ikiwa ni idadi ndogo zaidi, lakini tofauti ni kwamba lango la Yanga limelindwa na Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’kwa nyakati tofauti.

Akizungumzia clean sheet, Angban alisema ni jambo la furaha kwake na shukrani kwa wachezaji wenzake pamoja na uwezo binafsi anayopigana kuhakikisha anauonyesha awapo uwanjani.

“Ni jambo zuri, lakini siku zote haya ndiyo matokeo ya mtu binafsi na timu kwa ujumla. Siwezi kusema kuhusu ni clean sheet ngapi nifikishe kwa sababu ninacheza kwa kujituma kwa ajili ya timu yangu ili iendelee kufanya vizuri,” alisema kipa huyo.

Mechi Simba ilizoruhusu bao ni katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, ushindi wa 3-1 dhidi ya Ndanda na sare ya 1-1 na Yanga, huku ikizikazia Kagera Sugar (2-0), Mtibwa Sugar (2-0), Majimaji (4-0), JKT Ruvu (0-0), Azam (1-0) na Mbeya City (2-0).  


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV