February 13, 2017




Na Saleh Ally
HIVI karibuni, hatimaye Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lilitoa haki ya Watanzania baada ya kuitangaza timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika.

Serengeti Boys imefuzu Afcon baada ya Congo Brazzaville kubainika ilimchezesha mchezaji kijeba ambaye alifunga bao pekee walipoifunga Serengeti kwa bao 1-0 na kuwa wamevuka kwa mabao ya ugenini. Maana Dar es Salaam, Serengeti walishinda kwa mabao 3-2 hivyo jumla kuwa na sare ya mabao 3-3.

Baada ya Caf kutangaza, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliibuka na kusema wanahitaji kitita Sh bilioni moja ili kuisaidia timu hiyo kufanya vema.

Malinzi alikuwa akihitaji michango kutoka sehemu mbalimbali, kwa wadau wa michezo, soka na hata serikali. Mimi niseme, ninaunga mkono suala hilo la michango kama itawezekana. Lakini ninataka kujua, wao TFF wamejipanga vipi, wana kiasi gani mkononi ili wadau wajue kiasi gani kinahitajika.

Najua jukumu la kuiongoza timu hiyo ni lao na kuna fedha zimekuwa zikitoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya soka. Vifaa na mambo mengine ambayo kamwe wamekuwa wakikaa kimya bila ya kusema na wakati mwingine wakisema ni mambo ya TFF.

Kupitia hayo ndiyo maana naibuka na kusema lingekuwa jambo zuri kama TFF ingesimama na kutueleza kwamba kawaida inapata msaada wa kiasi gani na imeingiza kiasi gani.

Mtu kusaidia timu yake ya taifa ni fahari, lakini tunajua TFF ina jukumu la kuiendeleza na wamekuwa wakipokea fedha kadhaa kwa ajili ya maendeleo ya vijana na kadhalika.
Fedha za Taifa Stars ambazo zilikuwa zikitolewa na wadhamini Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) zilielezwa kuwa na mushkeri katika masuala ya mahesabu.

TBL walipeleka mkaguzi wa kwao kukagua fedha hizo. Kukawa na walakini mkubwa na hili TFF wanalijua na huenda kwa asilimia kubwa limechangia kampuni hiyo kujiondoa.

Kama unakumbuka, hata Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambalo hutoa dola 250,000 (zaidi ya Sh milioni 546.9), walilazimika kutuma watu wao kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mahesabu yao kama ilivyo kawaida yao, lakini mwisho ilionekana kuna tatizo pia.

Najua Fifa wanajua fedha zaidi katika masuala mbalimbali maendeleo ya soka, masuala ya ukarabati wa viwanja, ofisi, uendeshaji ofisi, soka la wanawake na kadhalika.
Kama TFF itakuwa inaomba msaada bila ya kuweka wazi kuhusiana na fedha ambazo wanazipata, kwangu naona si sawa hata kidogo.

Nitawauliza TFF, sasa wakati wa Serengeti Boys wanaweza kuwashirikisha wananchi ambao ndiyo wamiliki wa shirikisho hilo. Lakini fedha nyingine wanapopewa, kila kitu wamekuwa wakifanya mambo kimyakimya na walakini unakuwa wazi, si jambo sahihi.

Kuisaidia mimi nitajitahidi kuwa mmoja wao kwa kuwa ni timu yangu ya taifa na nina imani kubwa vijana hao ndiyo watakuwa nyota wa baadaye wa timu zetu na huenda watalibeba taifa na kwenda mbali zaidi.

Tulihitaji kuwa na mwanzo kama huo, vijana ambao wanahitaji kulelewa zaidi na sasa wamepata nafasi ya kujitangaza na kama watafanya vizuri kwenye michuano hiyo nchini Gabon, hakuna shaka kwamba watajitangaza na baadaye kutoka nje ya nchi yetu.

Tunahitaji wachezaji wanaocheza nje ya Tanzania ambao watajifunza mengi na baadaye kuwa msaada. Ushindani wa nchi nyingi hasa zile za Afrika Kaskazini au Ulaya ni mkubwa ukilinganisha na hapa nyumbani.

Kama vijana hao watapata nafasi, ikiwezekana hata timu nzima baada ya mashindano itakuwa ni msaada mkubwa kwetu hapo baadaye.


Hivyo, pamoja na yote hayo, naendelea kuwasisitiza kwamba TFF wawe wazi katika masuala ya fedha ili iwe rahisi kujua kinachotakiwa kuchangiwa ni kipi hasa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic