Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), limeitaka Klabu ya Young Africans ya Dar es Salaam kulipa mara moja deni la aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernst Wilhelmus Johannes Brandts - Raia wa Uholanzi waliyevunja naye mkataba miaka miwili iliyopita.
Klabu ya Young Africans imetakiwa kulipa dola 11,000 za Marekani kama ambavyo iliamriwa Juni 30, 2015 na Kamati ya Hadhi ya Wachezaji ya FIFA.
Kwa kuchelewa kulipa fedha hizo tangu Juni, 2015 Klabu ya Young Africans imeamliwa pia ilipe fidia ya asilimia tano ya deni halisi.
Young Africans wametakiwa kulipa fedha hizo na kutuma nakala ya malipo hayo, kabla ya shauri hilo halijapelekwa Kamati ya Nidhamu.
Kutolipa deni hilo kwa wakati, imetafsiriwa kwamba Klabu ya Young Africans imevunja Kanuni ya 64 inayozungumzia Nidhamu katika FIFA yaani FDC (FIFA Disciplinary Committee).
Klabu (Young Africans) inakabiliwa adhabu za kupigwa faini zaidi ya awali, kukatwa pointi katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea kwa sasa au kushushwa daraja.
Kamati hiyo ya Nidhamu inatarajiwa kukutana wakati wowote wiki ijayo na suala la Nidhamu ya Young Africans litakuwa ajenda ili kama Young Africans hawakulipa, watachukua hatua kama adhabu zinavyojieleza hapo juu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeagizwa haraka kufuatilia suala la deni hilo katika Klabu ya Young Africans na kurudisha majibu FIFA. TFF kupitia Katibu Mkuu, imeagizwa kupeleka barua ya FIFA katika Makao makuu ya Klabu hiyo, yaliyoko kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
TFF tumeliweka wazi suala hilo kama ‘Tahadhari kabla ya hatari’, kwani tungeweza kufanya mawasiliano kati ya shirikisho (TFF) na klabu (Young Africans) kwa siri tu, lakini ikitokea huko mbele klabu inakutana na adhabu mojawapo, lawama hushuka TFF kwa madai kwamba tumekalia taarifa muhimu ya kuchukuliwa hatua haraka.
Tunaagiza uongozi wa Young Africans, kulifanyia kazi jambo hilo mara moja kwa utekelezaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment