Mashabiki wa Simba leo wana kila sababu ya kuelekeza dua zao kuomba Yanga iwatandike Mbao FC katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.
Simba haijashiriki michuano ya kimataifa kwa misimu minne sasa, jambo ambalo linaonekana ni geni kwa timu hiyo ambayo imekuwa ikifanya vema katika hatua hiyo na kuonekana kama wawakilishi bora wa Tanzania ingawa sifa hiyo imepokwa sasa na watani wake, Yanga.
Tayari Simba imefuzu katika fainali ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza baada kuitwanga Azam FC kwa bao 1-0, jana.
Iwapo Yanga watashinda leo katika mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, maana yake kila kitu kitabaki kuwa cha timu hizo kongwe.
Yaani ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ubingwa wa Kombe la shirikisho utabaki kwa Yanga na Simba.
Kwenye Ligi Kuu Bara timu hizo ndiyo zinazofukuzana na Simba ikiwa kileleni lakini haina uhakika sana kama itabeba ubingwa huo kwa kuwa Yanga ambao ni watetezi wanaonekana kuwa na kasi kubwa.
Kayika Kombe la Shirikisho, kama Yanga akiingia fainali na kukutana na Simba, maana yake itakuwa rasmi timu hizo ndiyo wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa msimu ujao.
0 COMMENTS:
Post a Comment