Kipa namba moja wa Kagera Sugar, Juma Kaseja, ametamka kuwa maisha yake anategemea soka, hivyo hatasita kurejea kuichezea klabu yake ya zamani ya Simba kama ikimhitaji.
Kauli hiyo, aliitoa hivi karibuni mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba iliyopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera, matokeo yaliyomalizika kwa Kagera Sugar kushinda mabao 2-1.
Kipa huyo aliwahi kuichezea Simba na kuipa mataji kadhaa akiwa kama nahodha mkuu wa timu hiyo kabla ya kutimkia Yanga, Mbeya City na hivi sasa Kagera.
Kaseja alisema umri wake wa kustaafu kucheza soka bado, hivyo basi ataendelea kucheza hadi pale atakapoona ni muda mwafaka kwake kustaafu.
Kaseja alisema anashangazwa na maneno ya mashabiki wa soka wanaodai yeye ni mzee lakini hivi sasa ni tegemeo na mwezi Januari, mwaka huu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi.
“Bila ya kuwa mvumilivu basi ningepotea kwenye soka muda mrefu kutokana na maneno ya mashabiki wa soka, lakini nilijitahidi kuyaweka kando maneno yao na badala yake kupiga kazi ambayo leo hii naonekana kijana.
“Kama unakumbuka niliwahi kuitwa mzee, nauza mechi lakini kama ningekuwa ninauza mechi, basi ningewauzia hao Simba tuliocheza nao katika mechi hiyo ili wapate ushindi, maana si walikuwa wanataka ushindi ili wachukue ubingwa.
"Nikwambie tu, soka halipo hivyo kama wanavyofikiri, mimi maisha yangu ninayaendesha kwa ajili ya soka, na kuhusiana na taarifa za kurudi, mimi sina tatizo, hiyo ndiyo ajira yangu Simba wakinitaka narudi tu," alisema Kaseja.
0 COMMENTS:
Post a Comment