Shirikisho la Soka Tanzania au TFF, limefungua mashitaka kwa madai ya kutoheshimu na tayari atafikishwa kwenye kamati ya Maadili.
Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila mwanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.
Wanafamilia wa mpira wa miguu ni pamoja na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi wa mpira wa ngazi zote na waajiriwa wa taasisi ambazo ni wanachama wa TFF wa ngazi mbalimbali.
Ili kutunza heshima ya mpira wa miguu Tanzania, wanafamilia wa mchezo huo katika kutimiza masharti ya kanuni za maadili za TFF, hawana budi kuheshimu na kufuata taratibu zote hizo ndani na nje ya uwanja.
Taswira njema ya shirikisho inajenga imani ya wadau wakiwamo serikali, mashirika mbalimbali ya umma na binafsi, vyombo vya habari, vyama vya mpira vya kimataifa, NGO’s na watu binafsi kwa taasisi (TFF). Kinyume chake ni kulibomoa shirikisho.
Dhima ya uongozi wa TFF ni pamoja na kulinda na kutunza heshima hii. Hivyo vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjaji wa maadili havitavumiliwa, na vikitokea hatua zitachukulia.
Na kwa muktadha huu Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, limemfungulia mashtaka ya kinidhamu Msemaji wa Simba Bw. Hajji Manara kwenye Kamati ya Maadili. Leo hii Aprili 21, 2017 atapewa mashtaka yake na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa.
TFF inaendelea kutoa rai kwa wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza, kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya mpira wetu.
0 COMMENTS:
Post a Comment