Na Saleh Ally
KIPIGO cha mabao 3-2 kutoka kwa Barcelona ikiwa nyumbani, kimesababisha presha kubwa kwa Real Madrid katika suala la mbio za kuwania ubingwa wa La Liga.
Madrid wangependa kubeba La Liga ambayo wameikosa kwa zaidi ya misimu minne. Walikuwa na nafasi kubwa ya kufanya hivyo lakini sasa inaonekana ni finyu kabisa.
Tayari wanalingana pointi na Barcelona baada ya kipigo hicho pale Santiago Bernabeu. Kila timu ina pointi 78 lakini Barcelona ndiyo vinara kwa kuwa wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Madrid wao wana mechi moja mkononi kwa kuwa Barcelona kacheza mechi 34 na Madrid 33. Hii inafanya Madrid kuwa na mechi tano mkononi, tofauti na nne za wapinzani wao.
Lakini usisahau, ulichonacho ni kile ambacho tayari unacho. Unachokitarajia hauwezi kujua kinachofuatia. Hii inazidi kuipa Madrid presha zaidi katika kuwania ubingwa wa La Liga.
Ukiangalia katika mechi tano zilizobaki, utagundua pia ugumu unaonekana zaidi kwa Madrid na hakuna ujanja ni lazima wafanye kazi ya ziada tofauti na ilivyo kwa Barcelona.
Mechi tano za Madrid ndani yake kuna timu mbili kubwa na imara, hizo ni Valencia na Sevilla na zimekuwa zikiisumbua sana Madrid. Mbali na hiyo kuna Malaga na Celta Vigo ambazo ni tatizo pia kama hawatakaa vizuri.
Kwa upande wa Barcelona, mechi zake nne, kuna vibonde wawili, La Palmas na Eibar. Mechi moja ya “Barcelona Derby” ambayo wanakutana na wapinzani wao wakubwa katika Jiji la Barcelona na ile ya “Manyambizi” wa Villarreal ndiyo inaonekana kuwa ngumu angalau.
Madrid hawana ujanja, wanachotakiwa ni kushinda mechi zote tano huku wakiwa bado wana kumbukumbu ya kipigo hicho cha mabao 3-2 kilichoamsha ugumu na presha hiyo tofauti kama wangekuwa wanaizidi Barcelona pointi tatu na mchezo mmoja mkononi. Hii inampa wakati mgumu Kocha Mkuu wa Madrid, Zinedine Zidane ambaye amesisitiza, wanaweza kufanya vizuri zaidi wakati wa presha.
Pamoja na kuwa na majeruhi kadhaa akiwemo Gareth Bale, bado anaamini kikosi chake kitapambana na amekuwa akijaribu kuipoza presha ili isiharibu mambo.
Ukiangalia mechi nane za mwisho, Madrid wameshinda sita, sare moja na kupoteza moja na wamekusanya pointi 19 baada ya kufunga mabao 11 na kufungwa 12.
Wao Barcelona wameshinda sita pia, hawana sare na wamepoteza mbili na kukusanya pointi 18 baada ya kufunga mabao 13 na kufungwa 12.
Hii inaonyesha ni timu mbili zenye kiwango kinachofanana sana na nguvu inayokaribiana, hivyo ubingwa bado hauna mwenyewe.
Kocha wa Barcelona, Luis Enrique, yeye pia ana presha. Imezidi kuwa kubwa kwa kuwa anaamini ana nafasi kubwa ya kubeba ubingwa na kulitetea taji hilo.
Anachotaka Enrique ni kushinda mechi zote nne. Halafu litakuwa ni suala la kuangalia nini kitafuatia kwa wapinzani wao katika mechi zao.
Presha inaongezeka kwake kwa kuwa tu, tayari ametangaza kuachana na Barcelona. Hivyo angependa aondoke na taji hilo.
Hii ni kwa kuwa wameshang’olewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hawana nafasi tena ya kushiriki Uefa Super Cup wala Club World Cup. Si timu wanayotaka kuiona mashabiki na viongozi wa Barcelona.
Ndiyo maana presha ya kumaliza vizuri inamuandama na anachotaka ni ubingwa wa La Liga ambao utampa nafasi nzuri ya kuaga siku ya mwisho.
Soka ni burudani ya kushangaza. Lakini kila unapoitumikia, uchezaji wa karata ndiyo jambo muhimu zaidi. Ukikosea kuzicheza, burudani inageuka karaha au adhabu.
MECHI ZILIZOBAKI:
Barcelona (MECHI 4):
Espanyol, Villarreal, Las Palmas na Eibar
Real (MECHI 5):
Valencia, Granada, Sevilla, Celta Vigo na Malaga.
0 COMMENTS:
Post a Comment