May 12, 2017





Na Saleh Ally
NAFIKIRI ni vizuri kwenda moja kwa moja kuelezea kile ambacho nakiona kinataka kuchukua nafasi zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linakwenda kwenye uchaguzi mkuu.

Uongozi uliopo madarakani chini ya Jamal Malinzi umefeli mambo mengi sana ambayo uliahidi na kufanikiwa kwa asilimia kiduchu sana, pekee la kujifisifia ni Serengeti Boys kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika.

Tunakubaliana sote kwamba vyombo vya habari vimeungana kwa pamoja kuisifia TFF katika hili na baada ya hapo vimeungana na Watanzania wote kuomba ichangiwe.

 Kuna gharama kubwa inatumika kuhakikisha Serengeti Boys inachangiwa. Najua chochote mbele kitakua sifa ya mtu au kundi na si Watanzania wote walioshiriki.

Lakini wakati kuna hayo mafanikio kiduchu, vyombo vya habari na Watanzania wameungana na TFF kuhakikisha timu ya vijana wetu inafanya vema. Na shirikisho hilo linafurahia kabisa.

Hayo ni mafanikio kiduchu, tumeungana. Lakini kwenye sehemu ambayo ni mbovu na TFF imevurunda, TFF haitaki Watanzania waungane nayo na kusema ukweli kuhusiana na hilo. Haitaki kukosolewa au kuanikwa kwa kuelezwa linachofanyika kwamba si kitu sahihi.

Kwa kifupi, TFF inaona inaonewa linapofikia suala la kukosolewa. Ndiyo maana umeona kuna kikundi cha wale wanaoona wana faida, hawataki ikosolewe, hawakubali ielekezwe na wao wameamua “kumlinda bwana” bila ya kuchoka. Jambo ambalo mimi nalichukulia ni udhaifu wa juu kabisa.

Kuna mtu mmoja aliniambia kwamba kuna mpango wa “kuwalinda” na kuwapa nafasi hata ya safari wale watakaokuwa tayari kutetea kila jambo bila ya kujali makosa. Siwezi kuingia kwenye udhaifu huo na ninawashauri wanahabari kuangalia utaifa kwanza badala ya tamaa za mioyo yao.

Kama unakumbuka, hivi karibuni TFF ilitoa taarifa ikilalamika kusakamwa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kigezo kwamba ni kipindi cha uchaguzi, hivyo inasakamwa sana.

Ninachoamini ni kizuri, TFF pamoja na wale wanaotaka kuitetea bila ya kuangalia uzalendo, wajifunze jambo kwamba sasa ndiyo kipindi sahihi cha mahesabu ya miaka minne ya uongozi wa TFF. Hata wakati wa uchaguzi mkuu ni miaka mitano ndiyo kipindi cha kuibua hoja na kuhoji kuhusiana na ahadi au mwenendo wa uongozi.

Kama TFF haitaki ihojiwe sasa kwa kigezo cha uchaguzi, inataka ihojiwe vipi? Baada ya kurejea madarakani tena na kuendelea kutoa ahadi zisizotekelezeka?

TFF wanapaswa kujibu mambo kwa hoja, wanaweza kukosoa kwa hoja pia na si kutisha kwa kuwa wanakwenda katika uchaguzi, wakitumia neno wengine wanapigiwa kampeni.

Kukubali kujifunza ndiyo uungwana sahihi. Kama TFF imeonyesha wazi kuwa imefeli kwa asilimia kubwa, iwe tayari kujibu hoja.

Kama watu wameamsha hoja za ufujaji, kinachotakiwa ni kujibu na si kutisha. Kufanya hivyo ni dalili mbaya za kutaka kuyapeleka mambo katika njia zisizo sahihi zinazotaka kuwatisha waandishi na vyombo vya habari.

Hili si sahihi kwa uhuru wa wanahabari na vyombo vyenyewe lakini si sahihi kihisia kwa kuwa inaweza kusababisha kuzuka kwa hisia zisizo sahihi kutakapotokea jambo ambalo si sahihi.

Kama watu au wadau wanaiunga mkono TFF katika suala la Serengeti ambayo ni sehemu kiduchu ya kujivunia, basi TFF pia itoe nafasi watu wakosoe kupitia walipokosea.
Viongozi wa TFF nawakumbusha tena kwamba shirikisho hilo ni mali ya Watanzania. Wanapofikia wanawakosoa basi msikilize.

 Msikimbilie kusema mnachafuliwa wakati mnajua nyie si wasafi. Kama mnaona hivyo, basi nanyi muwe huru kuelezea badala ya kuonyesha ubabe jambo ambalo litachangia nyie kufeli zaidi.


SOURCE: CHAMPIONI LILILO MTAANI LEO

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic