Na Saleh Ally
KUWA mrefu ni sifa, mrefu ana nafasi ya kuona mbali zaidi lakini ajabu utaona urefu unaweza usimpe nafasi ya kuona vilivyo mbali zaidi.
Maana yake ni hivi, unaweza kuwa mrefu lakini ukawa hauna macho yenye uwezo mzuri. Maisha yana vigezo vipi kukamilisha neno bora, ndiyo maana hauwezi kuwa bora kwa kigezo kimoja.
Kipa Juma Kaseja alitua Simba mwaka 2002 akitokea Moro United aliyokuwa ameichezea kwa misimu miwili tu. Leo tayari Kaseja anaonekana ni mzee na watu walishamtoa kasoro, kwamba “ameisha”.
Kipa Gianluigi Buffon maarufu kama Gigi, sasa ana miaka 39 na Juni 3 panapo uzima atakuwa langoni akiipigania timu yake ya Juventus katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya mabingwa mara nyingi zaidi wa michuano hiyo, Real Madrid.
Buffon amecheza mechi 654 kwa ngazi ya klabu akiwa na Parma ambayo ilimlea hadi alipoanza kucheza katika Serie A na baadaye Juventus ambayo inaonyesha atamaliza soka lake.
Wachezaji wenzake katika klabu mbalimbali nchini Italia wamekuwa wakimuita “Maradona wa Makipa”. Hii inatokana na kumfananisha kuwa ni mwenye mafanikio zaidi unapozungumzia walinda milango nyota au wenye mafanikio zaidi.
Buffon au Gigi anatokea katika familia ya wanamichezo hasa. Mama yake, Maria Stella alikuwa nyota wa mchezo wa watupa vitufe, baba yake mzazi alikuwa ni “baunsa” akishiriki mchezo wa kuinua uzito.
Dada zake Guendalina na Veronica, wamekuwa wachezaji nyota wa mpira wa wavu hadi katika timu ya taifa ya Italia ya mchezo huo.
Kuna makipa wengi wazuri na bora duniani kama Iker Casillas, Emmanuel Neuer, Edwin van Der Sar au Peter Cech, lakini kwa waliobaki wote wanaocheza soka sasa duniani kote, Buffon ndiye kipa bora zaidi.
Tayari ana makombe karibu yote makubwa, kwa Italia amechukua yote na zaidi ya mara mbili au tatu kwa kila moja kama yale ya Super Cup Italia na mengine yote.
Akiwa na timu ya taifa ya Italia, amebeba ubingwa hadi Kombe la Dunia mwaka 2006 lakini anapambana na Ligi ya Mabingwa Ulaya aliyowahi kuingia fainali mara mbili lakini akatoka mikono mitupu.
Mtoto huyo wa baunsa hachoki na ubora wake haushuki na sasa amekuwa ni kocha ndani ya uwanja na mchezaji anayekubalika na timu zote kila zinapokutana na Juventus.
Bado ana imani ya kuwazuia akina Cristiano Ronaldo, Karim Benzema na vijana wao ili atimize ndoto yake.
Wakati anapambana uwanjani, Buffon ana sifa nyingi ambazo ni wachezaji wachache wa Kitanzania hawawezi kuwa nazo na hapa nitarudia ule mfano wa mtu mrefu asiyeona mbali.
Kwamba kwa wachezaji wengi wa Tanzania husubiri hadi wanapostaafu ndiyo waanze biashara. Wengi wamekosea na wanaishia kulalamika kwamba hakukuwa na kuwajali.
Wengi wa Ulaya, huangalia mbele zaidi na maisha ya baada ya soka. Miaka 10 katika soka la ushindani huwa ni mingi sana. Ndiyo maana tunamshangaa Buffon anayeendelea kushinda kwa miaka 22 mfululizo bila ya kuchuja. Huyu kweli si mtu wa kawaida.
Wakati akiwa ameanza kucheza Serie A, Mbwana Samatta ambaye ni nyota zaidi kuliko wachezaji wengine wa Tanzania ndiyo alikuwa ana miaka mitatu tu. Kumbuka Edibily Lunyamila ndiyo alikuwa kidato cha tatu.
Bado Buffon anaendelea kufanya vizuri zaidi, yeye ni nyota zaidi, lakini hata Lunyamila amemkuta na amestaafu na kumuacha akiendelea kufanya vizuri.
Anang’ara uwanjani lakini ana akili ya maisha, maana anajiendeleza na biashara kwa kiwango kikubwa.
Buffon ndiye mchezaji pekee aliyewahi kushinda uongozi wa Shirikisho la Soka la Italia (AIC), Mei 7, 2012 alitangazwa kuwa makamu wa rais wa shirikisho hilo huku akicheza. Akaweka rekodi ya kuwa mchezaji na kiongozi wa shirikisho.
Zaidi amekuwa akichuana na Casillas ambaye pia amemuacha akiendelea kung’ara.
Katika biashara Julai 2010, aliinunua timu ya Carrarese akimiliki hisa asilimia 50. Nyingine 50 zilibaki kwa bilionea Cristiano Lucarelli. Baadaye aliuza hiza zake kwa Maurizio Mian na kubaki na 20% tu. Msimu wa 2014-15 aliuza kila kitu na kuachana na Carrarese.
Mei 2011 aliingia kwenye bodi ya wakurugenzi au wamiliki wa kampuni kubwa ya Zucchi Group S.p.A., akiwa na hisa asilimia 19.4%. Baadaye ikitaka kufilisika, ilielezwa alitoa pauni milioni 20 kuinusuru.
Pia amewahi kumiliki kampuni nyingine kadhaa na amekuwa akijiwekeza kupitia kampuni mbalimbali kuonyesha anaamini ubora wake lakini anaamini maisha baada ya soka.
Kwa mchezaji wa Tanzania na wewe shabiki, jifunze anakopita Buffon halafu utatafakari. Kwa mchezaji peke yako, una chochote unaandaa katika maisha baada ya soka au unaamini kwa urefu wako utaweza kuona kila kilicho mbali hata uwezo wa macho yako kuina mbali utakuwa mdogo?
0 COMMENTS:
Post a Comment