Beki wa Simba, Abdi Banda amefunguka kuwa, kwa sasa amesimamisha mazungumzo na mabosi wake hao juu ya kuongeza mkataba mpya ambapo suala hilo litaendelea mara baada ya ligi kufikia ukingoni.
Beki huyo kwa sasa amebakiza muda mfupi kabla ya kumaliza muda wa kuitumikia timu hiyo tangu alipojiunga nayo akitokea Coastal Union ya Tanga huku akisaini mkataba wa miaka mitatu.
Banda amesema amesitisha mazungumzo hayo na anachokiangalia ni kupanga mipango na kuisaidia timu yake katika mechi zilizobakia watwae ubingwa kisha wapate muda wa kuweza kufanya mazungumzo.
“Mtazamo wangu ni kwenye mechi zetu mbili tulizobakiza za ligi ili kuona ni jinsi gani tunaweza kufanya vyema kwa kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo ambapo kwa sasa ushindani ni mkubwa kutoka kwa Yanga.
“Kwa sasa nimesitisha mazungumzo ya aina yoyote kwa ajili ya kuongeza mkataba mwingine wa kuitumikia Simba hadi ligi itakapoisha kwani michezo iliyobakia ni michache lakini ligi ikiisha tutapata muda wa kutosha kuweza kuzungumza.
“Kuhusu suala la kwenda kucheza soka Afrika Kusini, nadhani jambo hilo tuliweke pembeni kwani nikizungumzia kipindi hiki nitakuwa nawachanganya mashabiki, ni vyema kwanza tukamalizana na hili ambalo lipo mbele yetu,” alisema Banda.
0 COMMENTS:
Post a Comment