Nahodha na mshambuliaji wa Azam, John Bocco, ameweka bayana kuwa kadi nyekundu aliyopata kiungo wao, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ndiyo ilichangia kwa kiasi kikubwa wao kupoteza mechi yao na Simba kutokana na kulazimika kubadilisha mbinu ambazo zilisababisha washindwe kuipenya safu ya ulinzi ya wapinzani wao hao.
Kiungo huyo, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ alipewa kadi nyekundu dakika ya 16 ya kipindi cha kwanza na mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kabla ya Mohammed Ibrahim ‘Cabaye’ wa Simba kupewa kadi nyekundu dakika ya 76.
Azam inayonolewa na Mromania, Aristica Cioaba, juzi Jumamosi iliondoshwa katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kufungwa na Simba kwa bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar.
Bocco amesema kuwa Sure Boy ndiye aliyewagharimu kwa kiasi kikubwa kutokana na kadi yake hiyo ambapo iliwalazimu kubadilisha mfumo waliokuwa wakiutumia na kusababisha kushindwa kutengeneza nafasi za kuifunga timu hiyo.
“Tulianza vizuri na tuliwabana Simba lakini baada ya Sure Boy kupata kadi nyekundu kila kitu kwetu kilibadilika na kutulazimu kucheza kwa tahadhari na hata mashambulizi tuliyokuwa tunayapanga yakafa kwa sababu ya kuhofia kufungwa maana tulikuwa pungufu.
“Hatuna la kufanya kwani tushatolewa kwenye mashindano haya na pia hatuna kitu chochote cha kugombea zaidi ya kupigania kumaliza kwenye nafasi za juu kwenye ligi na kujipanga kwa ajili ya msimu nujao,” alisema Bocco.
0 COMMENTS:
Post a Comment