Kipa namba moja wa Simba, Daniel Agyei, raia wa Ghana, ameweka rekodi ya kipekee kwenye michuano ya Kombe la FA baada ya kucheza dakika 360 ambazo ni sawa na mechi nne bila ya kuruhusu bao.
Agyei ambaye amejiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo msimu huu, amefanikiwa kuweka rekodi hiyo walipocheza dhidi ya Polisi Dar, African Lyon, Madini FC na Azam FC huku akiisaidia timu yake kutinga fainali ya michuano hiyo ambapo watacheza dhidi ya mshindi wa mechi ya jana kati ya Mbao na Yanga.
Simba ilicheza na Polisi Dar katika hatua ya 32 Bora na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, hatua ya 16 Bora wakacheza dhidi ya African Lyon na kushinda 1-0, robo fainali wakaifunga Madini 1-0, kisha nusu fainali wakailaza Azam kwa bao 1-0.
Katika timu nne zilizocheza nusu fainali ya michuano hiyo ambazo ni Azam, Mbao Simba na Yanga, Simba pekee ndiyo kipa wao hakufungwa hata bao moja, huku makipa wa timu nyingine wakiruhusu mabao.
Kutokana na rekodi hiyo, Agyei amesema: “Ni jambo zuri sana kuona unamaliza mechi bila ya kuruhusu bao, kama nimeweza kufanya hivyo kwenye michezo iliyopita, basi nitafanya juhudi kubwa kuhakikisha hata mchezo wa fainali nisifungwe ili kuiweka vizuri rekodi yangu.
“Lakini ikitokea bahati mbaya nikaruhusu bao, nitawaambia wenzangu tupambane ili kuhakikisha tunaibuka na ushindi siku hiyo.”
0 COMMENTS:
Post a Comment