May 1, 2017Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema kuwa bado malengo yake hayajatimia licha ya kuwa baada ya kutinga fainali ya Kombe la FA juzi, ana asilimia kubwa ya kupanda ndege kwenda kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

Kauli hiyo, aliitoa mara baada ya timu yake kutangulia kwenye hatua ya fainali ya Kombe la FA kwa kuwafunga Azam FC bao 1-0 juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba itakuwa na uhakika zaidi wa kushiriki michuano ya kimataifa kama Yanga ilifanikiwa kuifunga Mbao FC katika mchezo huo wa FA jana CCM Kirumba, Mwanza.

Omog amesema malengo yake yeye ni kuhakikisha anaipa Simba makombe yote wanayoshiriki likiwemo la Ligi Kuu Bara na la FA.

Omog alisema, kikubwa atakachokifanya yeye hivi sasa ni kuhakikisha anashinda kila mchezo utakaokuwa mbele yake ili kufanikisha malengo yake.

“Nimeona mashabiki na viongozi wa Simba wakifurahi kuwatoa Azam katika mechi ya nusu ya fainali ya FA na kupata uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa kama Yanga wataifunga Mbao.

"Lakini kwangu mimi bado sijatimiza malengo yangu niliyojiwekea ya kuchukua makombe yote tunayoshiriki, la ligi kuu na hili la FA. "Nishawaambia wachezaji wangu tayari kwa kuwapa tahadhari mapema ya kutoridhika na hatua hii tuliyofikia na badala yake tunahitaji makombe kama unavyofahamu muda mrefu Simba haijachukua ubingwa," alisema Omog.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV