Si unajua amerudi, na amesaini Kagera Sugar, nina maaha yule beki aitwaye Juma Said Nyosso.
Nyosso amesaini Kagera Sugar mkataba wa miezi 24, amesisitiza amebadilika na sasa amekuwa mtu mwema lakini amepiga kijembe kwa kusema waliodhani ameisha wakutane uwanjani waone uwezo wake.
Mapema wiki hii Kagera Sugar chini ya Kocha Mecky Maxime ilimsajili Nyosso akiwa ametoka kwenye adhabu ya kufungiwa miaka miwili kwa kosa la kumdhalilisha aliyekuwa nahodha wa Azam FC, John Bocco. Wakati huo Nyosso alikuwa akiichezea Mbeya City.
Wakati Nyosso anafanya kitendo hicho katika mchezo namba 32 wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015/16 kati ya Azam na Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, mechi hiyo, Azam ilishinda mabao 2-1.
Nyosso amesema anafurahia kumaliza adhabu yake na sasa anarejea uwanjani akiwa amejifunza vitu vingi na hawezi kurudia kufanya vitendo vya udhalilishaji.
“Nimefurahi kujiunga na Kagera Sugar, nimerudi kupiga kazi na hivyo sitazungumza kwa mdomo bali vitendo, hivyo mtu yeyote atakayetaka kuona uwezo wangu, tukutane uwanjani.
“Muda wote niliofungiwa adhabu ilikuwa ikiniumiza moyoni, sasa mimi ni mtu mpya na nilikuwa nafanya mazoezi ya nguvu ndiyo maana nasema sasa ni kupiga kazi tu.
“Namshukuru Mungu kwanza kwa kuniwezesha kumaliza adhabu hii lakini kama unavyojua mimi siku zote huwa siyo msemaji sana katika vyombo vya habari, mimi kazi tu,” alisema Nyosso.
0 COMMENTS:
Post a Comment