June 14, 2017Kiungo Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya amefunguka kuwa, mara baada ya kutua nyota wa Uganda, Emmanuel Okwi katika timu hiyo atamwachia jezi yake namba 25.


Okwi ni miongoni mwa wachezaji ambao wanatarajia kutua katika klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ambapo uongozi wa timu hiyo umejipanga kumalizana naye kwa dau la dola 50000 (Milioni 110).

Aidha wakati mshambuliaji huyo wa Kiganda alipokuwa akiitumikia Simba kwa kipindi chote alikuwa akivaa jezi namba 25 hadi alipoachana na klabu hiyo, hivyo ni wazi kuwa iwapo atarejea atahitaji kuivaa jezi yake hiyo.

Kichuya ambaye kwa sasa anavaa jezi hiyo amesema kuwa, yupo tayari kuachana nayo mara baada ya Okwi kutua na iwapo ataihitaji na yeye kuvaa namba yeyote ile atakayopewa.

“Mimi sina shida iwapo Okwi atatua Simba na kuitaka jezi yake, nitakuwa tayari kumwachia na mimi nivae namba yeyote ile nitakayopewa kwani sina shida huwa siangalii sana vitu kama hivyo na ninachokiangalia ni kuona najituma kwa ajili ya timu hivyo namba yeyote nikipewa ni sawa.


“Nawakaribisha wachezaji wote wanaosajiliwa lakini kwa sasa ni mapema kusema kuhusu kuwania namba kwa kuwa bado sijawaona lakini lengo ni kuona naendelea kuwa bora msimu ujao,” alisema Kichuya.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV