Kipa Aishi Manula amethibitisha kwa mdomo wake kuwa anaondoka Azam FC na kutua Simba huku akitaja sababu tatu za kuchukua uamuzi huo.
Kipa huyo amesema hatasaini mkataba mpya na timu hiyo baada ya huu wa sasa unaoisha Julai 31, mwaka huu kumalizika, na chaguo lake la kwanza ni kutua Simba ambayo imeshamuandalia mkataba wa miaka miwili.
Manula amesema anaondoka Azam kutokana na mabosi wa timu hiyo kutothamini kile anachokifanya, pia dau dogo la usajili pamoja na timu hiyo kutokuwa na nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
“Sitasaini mkataba mpya na Azam baada ya huu wa sasa kufikia tamati Julai 31, mwaka huu, naamua kuondoka kwa sababu viongozi hawathamini uwezo wangu, kwa sababu licha ya kujitoa kwa uwezo mkubwa lakini eti wananiwekea dau la usajili chini ya milioni 20, hiyo inadhihirisha wazi kwamba hawajali ninachokifanya.
“Niwe muwazi kwamba mimi nilikuwa nacheza Azam kwa mapenzi yangu yote bila ya kuangalia juu ya kile ninachokipata lakini kwa hili ambalo wamenifanyia, naona kabisa siwezi kuendelea kucheza hapa, kwa sababu thamani yangu wameishusha sana tofauti na ambavyo nilikuwa nafikiria.
“Lakini pia naondoka Azam kwa sababu timu haishiriki michuano ya kimataifa kwa msimu ujao, kwa hapa nilipofikia siwezi kucheza timu ambayo haishiriki michuano ya kimataifa, ukiangalia mimi ni kipa wa timu ya taifa, hivyo ni lazima nionekane na sehemu kubwa ya Afrika.
“Najua kuna timu zinanifuatilia na baadhi yao tayari nimeanza kuzungumza nazo. Lakini kipengele cha kwanza ambacho nimekiweka ni lazima nihakikishiwe nafasi ya kuanza ndani ya kikosi cha kwanza halafu ndiyo mambo mengine yafuate,” alisema Manula.
Tayari Manula amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili na ameondoka rasmi Azam FC ambayo alianza kujulikana akiwa nayo.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment