June 12, 2017Na Saleh Ally
NIANZE kukuambia kama vipi tueleze faida ya kambi ambayo timu ya taifa, Taifa Stars walikwenda kuweka huko nchini Misri, wamerejea nchini na kushindwa kupata ushindi hata dhidi ya Lesotho.

Wamekwenda kuweka kambi Misri, jambo ambalo mimi niliamini walikuwa hawana sababu kwa kuwa hata hapa nyumbani kuna sehemu nyingi za kufanya hivyo maana hakukuwa na mechi ya kirafiki ambayo huenda ingekuwa sababu ya kusema lazima waweke kambi huko Misri.

Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na hiyo kambi ambayo moja kwa moja siipingi, lakini bado nasisitiza hakukuwa na sababu na sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho inaonyesha haikuhitajika.

Huenda unaweza kusema wachezaji walitakiwa kuhamasika, lakini hawajaonyesha hiyo hamasa na mwisho tumeangukia hapo.

Pia unaweza kujiuliza kuhusiana na kambi nchini Misri kwa sababu ya Lesotho ambayo tumeshindwa hata kuifunga. Lakini vipi itakuwa hapo mbele tutakapokutana na Uganda na baadaye Cape Verde?

Tutakwenda Ujerumani au Hispania kwa ajili ya kambi kwa ajili ya kuwaonyesha wachezaji kuwa mechi inayofuata ni ngumu zaidi.
Kama watabaki hapa nyumbani na maana ya kambi ilikuwa ni hamasa, maana yake ujumbe wanaopelekewa ni kwamba mechi inayofuata si ngumu sana kama ile iliyopita.

Sitaki kuibeba Lesotho, lakini wewe kocha au mchezaji au kiongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nakuuliza hivi; hivi sisi Tanzania nani tukikutana naye tunakuwa angalau na asilimia 55 ya ushindi? Kwamba “hawa wetu”.

Hata wachezaji, najua mtasema mpira unadunda, najua mtasema hata ninyi mlitaka ushindi, nakubaliana nanyi kabisa. Lakini niwaulize, haya mambo ya kufanana tokea nyie mkiwa shule za msingi au sekondari, hadi leo mnacheza na yanaendelea kuwa yaleyale, kweli Watanzania wana mioyo ya kuendelea kuvumilia tu? Watavumilia hadi lini?

Kila mechi ni ngumu na mimi ninawatia moyo kwamba tunaweza kuamka na kufanya vizuri mbele. Lakini lazima tukubaliane nanyi kwamba lazima mfanye kazi ya ziada na kama mnajituma asilimia mia, mjue mnahisi na hamjafikia.

Tumechoka kuwa wachovu, tumechoka kuonekana walaini na Watanzania hawajisikii ukubwa, uimara na watu wanaoogopwa linapofikia suala la soka. Maana hata Somalia ambao huandalia timu yao Nairobi, Kenya, nao huona Tanzania ni saizi yao wanapokutana nayo.
Kweli kulaumu sana si vizuri lakini mimi nawaelewa Watanzania wengi wapenda soka kwamba wamechoka. Vizuri pia tukawaelewa na kukubali kwamba, jamani hawa watu wamevumilia sana.

Nani anaweza kukataa leo kuwa Watanzania wamechoka kuvumilia au wamevumilia sana? Waungwana unachokipenda ukiona hakikufurahishi, basi kinageuka karaha.

Badala ya wachezaji, makocha au TFF kuanza nanyi kulalama kwa kuona kuwa mnajitahidi sana lakini mnalaumiwa, basi badilisheni gia na muanze kushinda.

Timu ya taifa ni yetu sote, kila aliye hapo amepewa jukumu la kuisaidia. Hivyo nyie mmepewa jukumu hilo mkiwa sehemu ya Watanzania. Mkiona hamuwezi pia mnaweza kuondoka na wengine wakapata nafasi hiyo.

Nianze na TFF, kama imeshindikana, Rais Jamal Malinzi na timu ya marafiki zako, manaweza kukaa kando. Maana maendeleo hayawezi kuwa maneno tu.

Kocha Mkuu, Salum Mayanga na benchi la ufundi, Watanzania wanataka ushindi kwa kuwa inaonekana mmehudumiwa na hamna mnachofanya.

Wachezaji nanyi, lazima mjue thamani za jezi mnayovaa na ikiwezekana mnaweza kuwa kizazi cha kubadili mambo kutoka katika “miaka ya kubahatisha” hadi timu yenye nafasi ya kufanya vizuri.

Wengine tokea tunasoma miaka ya 1990, hadi leo tuna familia zetu kila kukicha ni maumivu tu na Stars. Halafu hamtaki watu waseme. Tokea kina babu hadi wajukuu, hakuna nafuu. Tumechoka, tutawaunga mkono kama mtabadilika, ikishindikana basi tutapambana kuhakikisha mnawapa nafasi wanaoweza kubadili mambo.


Hii ni timu ya taifa, mnapaswa kuonyesha utaifa badala ya kufanya mambo kama mpo kwenye klabu zenu.

1 COMMENTS:

  1. Ha Jamaa wa TFF Kutafuta kingilio tu wewe unapeleke misri timu ya taifa kwa sababu gani. Halafu wachezajia wanasema uwanja ulikuwa mdogo kwani TFF haikujua kwamba mechi itachezwa katika uwanaja wa Azam
    Hawa TFF ndio wanatutia aibu tumuombe rais Mh J P Magufuli kutumbua majipu hayo aletwe Rais wa TFF mwenye uchungu na nchi kwenda mbele kimpira

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV