June 12, 2017


Na Saleh Ally
WAKATI Romelu Menama Lukaku alipoingia katika ofisi ya Kocha Jose Mourinho kumuuliza kama ni kweli amekubaliana naye aondoke, jibu la kocha huyo Mreno lilikuwa ni fupi sana; “kila la kheri”.

Kauli hiyo ya Mourinho ilimfanya Lukaku aamini sasa hana ujanja, ni lazima aondoke Chelsea na kwenda Everton kwa mkopo na baadaye akachukua uamuzi wa kujiunga na timu hiyo.

Kuna ushauri mbaya wa Mourinho ambao unaonekana kuisumbua Chelsea, leo. Kwamba wakati wakimuuza Lukaku kwa pauni milioni 28 (zaidi ya Sh bilioni 78), Everton ilitaka ipunguziwe bei ili kama itafikia siku nyingine Chelsea wanamtaka basi kipengele cha “kurejea” kifanye kazi, ambacho kingeisaidia na Chelsea kupata nafuu.

Mourinho aliishauri klabu kuchukua mkwanja kwa kuwa alitaka fedha nyingi asajili kikosi bora na tayari Atletico Madrid ilikuwa imekubali kumuachia Diego Costa kwa kitita cha pauni milioni 32 (zaidi ya Sh bilioni 89).

Lukaku alikubaliana na Mourinho, hakuwa na maneno mengi na aliamini miaka 20 ni nafasi kubwa kwake kutengeneza njia sahihi.

Hakuna ubishi kwamba alikuwa anaumia kwa kuwa tangu anatokea kwao Ubelgiji, mara ya kwanza alipofika London kutembelea Uwanja wa Stamford Bridge alisema: “Uwanja mzuri sana, siku ikitokea ndiyo ninacheza hapa, kwa mara ya kwanza nitalia kwa furaha, ninaipenda sana Chelsea.”

Lukaku anaipenda Chelsea, alipojiunga nayo alijua safari ya mafanikio imeanza. Kuachiwa aende, halikuwa jambo rahisi kwake lakini hakuwa na ujanja kwa kuwa Mourinho alikuwa na mipango na asingeweza kusubiri.Asingeweza kusubiri kwa kuwa aliona Lukaku ni kinda, Mourinho anataka “watu wa kazi”. Wakati huo Lukaku alikuwa anajifunza, hivyo ilikuwa ni lazima kumuachia.

Leo, Mourinho naye ametangaza kumtaka Lukaku katika kikosi chake cha Manchester United. Hali inayowashangaza wengi lakini ukweli ni kwamba, mshambulizi huyo kutoka DR Congo wakati huo Zaire, sasa anaonekana ni “mtu wa kazi”.

Lukaku angekuwa Mtanzania kama mimi au wewe, huenda nafasi ya kupiga hatua ingekuwa ndogo na ingewezekana kabisa hata pale Everton angefeli na safari ikawa ni kurejea kwao Ubelgiji.

Wako wachache wanaweza kulingana naye na kuwa na moyo wa chuma, hakuna kukubali kushindwa!


Lukaku ambaye anasikia na kuzungumza Kiswahili hakuwa na muda wa kumlaumu Mourinho, badala yake alichoangalia ni kipi cha kufanya. Ndiyo maana leo ni mmoja wa wachezaji wachache katika gumzo la usajili na sasa Chelsea inaweza kutoa pauni milioni 75 hadi 100 ili kumpata.

Chelsea inaonekana imenuia kumpata kwa kuwa tayari Kocha Antonio Conte amemtaarifu mshambulizi Costa kwamba hamhitaji kwa ajili ya msimu ujao. Nafasi hiyo atakayeiziba kwa asilimia 99, inaonekana ni Lukaku.

Kwa maana ya kipaji, Lukaku anacho kwa kuwa baba yake mzazi Roger Lukaku amewahi kuichezea timu ya taifa ya Zaire sasa DR Congo. Mdogo wake aitwaye, Jordan alifanya vizuri katika akademi ya Anderlecht, sasa anakipiga Lazio ya Italia na binadamu yake, Boli Bolingoli-Mbombo ni tegemeo katika moja ya timu kubwa za Ubelgiji, Club Brugge.

Leo Lukaku anachagua tu, maana Man United imekubali kutoa pauni 200,000 (Sh 558m) katika mshahara wake kwa wiki, lakini yeye bado anaonekana angependa mshahara hata ukiwa chini ajiunge na Chelsea.Sasa tuanzie hapo, kwa nini Lukaku anachagua? Leo anakuwa na uwezo wa kuamua aende timu ipi kati ya Chelsea au Man United. Hizi ni timu kubwa kila mchezaji duniani angependa kuzitumikia kutokana na mafanikio yanayopatikana.

Lukaku anachagua kwa kuwa aliweka maneno kando, akatanguliza vitendo. Usisahau ni miaka mitatu tangu ameondoka Chelsea aliyokuwa anaipenda. Leo ni gumzo na tegemeo.

Kama atarudi Chelsea au atajiunga na Man United, kokote atapokelewa kama mchezaji tegemeo. Hili ndilo tunapaswa kujifunza.

Hapa nyumbani Tanzania, wengi mngefeli lakini anayeweza kuwa na moyo wa chuma huenda ni mshambulizi Mbaraka Yusuph, huyu anaweza kuwa mfano kidogo wa huo. Kwani baada ya kuondoka Simba akionekana uwezo si ule unaohitajika, sasa amekuwa tegemeo na umeona kabla hajajiuka na Azam FC, Simba na Yanga wote walikuwa tayari kumsajili.

Lazima ujifunze, unapokuwa hutakiwi, basi kuna jambo. Lipi, jiulize lakini lenga katika kujiendeleza, kujikuza na kuwa bora badala ya malalamiko kama ambavyo wamekuwa Watanzania wengi.

Kwa Mbaraka, hakuwa akitakiwa Simba kwa kuwa waliokuwepo walikuwa na uwezo mkubwa kwa maana ya mambo mengi ikiwemo uzoefu. Hii ni kama Mourinho alivyotaka kumsajili Costa akiona ana uzoefu na tayari ana majibu mzuri kuliko Lukaku, hakika alikuwa sahihi.

Lukaku amejikuza, Mbaraka amepambana kuonekana. Kocha yeyote anaweza kusema anawahitaji. Wako makocha wa aina nyingi na wengi wasingependa kukuza, badala yake kupata kilicho tayari. Kama ni mshambulizi, akimuweka first eleven, anachokwenda kufanya ni “mauaji” tu!

Kujipima na kukubali mambo wakati mwingine ni jambo jema kuliko kuhisi umeonewa na kufa moyo. Lukaku au hata Mbaraka wangefanya hivyo. Sasa wasingekuwa hapa walipo.


Tukubali, walipopitia wao ni somo kubwa na wanaweza kutusaidia kujifunza hata katika maisha ya kawaida ingawa walipofikia sasa, ndiyo wanakuwa na deni zaidi kwa kuwa wanatakiwa kuonyesha kilichowafanya watakiwe na wanaoonekana wakubwa kwa kuwa siku zote, wanataka makubwa tu. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV