NA SALEH ALLY
MICHUANO ya SportPesa Super Cup ilikuwa ni ya muda mfupi sana na ilifanyika katika kipindi ambacho ninaamini hakikuwa sahihi hasa kwa timu za Tanzania.
Ilifanyika wakati timu za Tanzania zimemaliza ligi na wachezaji wakitaka kwenda mapumziko, wengine wakiwa wameteuliwa katika timu ya taifa.
Kwa baadhi ya timu kama Simba na Yanga zilitoa wachezaji wengine kwenda katika timu za taifa za Rwanda, Burundi na Zimbabwe. Hivyo haikuwa rahisi sana kuwa na timu imara.
Gor Mahia na AFC Leopards za Kenya, hazina wachezaji wengi sana katika timu za taifa. Lakini zilikuwa bado na mwendelezo wa ligi.
Hivyo ikaonekana kama timu za Tanzania hazikuwa na nafasi nzuri ya kushinda au kufanya vizuri. Msimu ujao, huenda kuna haja ya kuangalia muda mwafaka hata kama itakuwa inafanyika nchini Kenya.
Binafsi naona ilikuwa moja ya michuano iliyofanikiwa sana licha ya kuwa ni ya muda mfupi. Ilipangiliwa vizuri na waandaaji au wadhamini SportPesa walionekana ni watu waliotaka kuona mambo yanakwenda katika mstari.
Bingwa wa SportPesa amechukua dola 30,000 (zaidi ya Sh milioni 65). Angalia michuano hiyo ya muda mfupi, timu inaweza kuingiza kiasi hicho cha fedha.
Kama haitoshi, bado bingwa anapata nafasi ya kucheza na Everton ya England. Kumbuka hii ni timu ambayo imeshiriki Ligi Kuu England kwa misimu mingi zaidi ya timu nyingine zote. Kwa klabu yoyote Afrika, hii inakuwa ni nafasi bora kabisa.
Baada ya michuano hiyo, nilidhani ulikuwa ni wakati mzuri wa kuwashukuru SportPesa kwa hicho ambacho wamekifanya kwa mpira wa Tanzania au Afrika Mashariki.
Badala yake nimeanza kuona tunawaingiza katika mjadala ambao kwangu, niwe wazi tu hauna msingi kabisa.
Nilipata taarifa kuwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), limekuwa likihoji kwamba halitakuwa jambo zuri kwa timu za England na Kenya kucheza mechi ya kirafiki hapa nyumbani Tanzania.
Inawezekana ni kutofuatilia mambo, hili linawezekana kabisa na wala hakuna shida hata kidogo. Hivi karibuni, Al Ahli ya Saudi Arabia ilisafiri hadi Qatar kucheza mechi ya kirafiki na Barcelona ya Hispania. Timu zote zilikuwa ugenini lakini mdhamini wao mkuu, Qatar Airways ndiye alikuwa mwenyeji wao.
Lakini hili la Super Cup ni rahisi zaidi kwa kuwa kila kitu kilikuwa wazi. Kwamba bingwa ndiye atacheza na Everton na timu zote ziliingia mashindanoni zikilijua hilo.
Kitu kizuri zaidi, kila nchi ilikuwa na uwiano mzuri wa timu kwa maana kila moja ilitoa timu nne. Tanzania ilikuwa na Simba, Yanga, Singida United na Jang’ombe Boys wakati Kenya walikuwa na timu za Gor Mahia, AFC Leopards, Tusker na Nakuru All Stars ambayo ni ya daraja la kwanza.
Achana na idadi hiyo ya timu, mechi zilichezwa nyumbani Tanzania. Lakini mwisho, timu za Kenya ndiyo ziliingia fainali na sasa moja ina uhakika wa kucheza na Everton. Ni sahihi kutaka kubadili hili?
Kama tunataka kubadili tunatumia ubabe na kweli tunaamini tutakuwa tunazisaidia timu zetu ambazo ziliwekewa kila kitu mezani zikashindwa zenyewe.
Timu zetu zimeshindwa hata kutupia kijiko kwenye sinia na kupeleka mdomoni. Sasa tunataka kuzilisha?
Ushauri wangu tuonyeshe Watanzania katika michezo tunaweza pia kufanya mambo kwa kufuata weledi na kusimamia makubaliano.
Vizuri tukaacha mechi ya Gor Mahia na Everton ichezwe hapa nyumbani na sisi twende tukapate burudani na kujifunza pia.
Kama timu zetu ziko makini, msimu ujao timu moja ibebe ubingwa na sisi tutasafiri kwenda Nairobi timu moja kutoka Tanzania ikicheza na timu ya England.
0 COMMENTS:
Post a Comment