Beki kinda wa Simba, Abdi Banda ameibuka na kusema amelazimika kukataa dau la Sh milioni 65 kutoka kwa uongozi wa timu yake kwani anataka kwenda Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa.
Banda amemaliza mkataba wa kuitumikia Simba mwishoni mwa msimu uliopita ambapo hatarajii kuongeza mkataba mwingine wa kuitumikia timu hiyo.
Banda amesema kuwa, alikataa dau la Sh milioni 65 ambalo Simba walipanga kumpa ili asaini mkataba mpya, kwani lengo lake ni kwenda kucheza nje.
Klabu ambazo beki huyo anatarajia kwenda kufanya majaribio Afrika Kusini ni Polokwane na Chipa United huku akiwa na mpango wa kwenda Australia kufanya majaribio pia.
“Nilifanya mazungumzo na Simba ambao walikubali kunipata Sh milioni 65 lakini nilikataa ofa hiyo kwa kuwa nahitaji kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na naamini fedha hizo nitazipata zaidi huko.
“Nitakwenda kufanya majaribio mara baada ya michuano ya Cosafa ambapo nitabaki huko huko Afrika Kusini sitarudi na timu ya taifa kwani nahitaji kujaribu bahati yangu,” alisema Banda.
Banda kesho Jumapili anatarajiwa kuingia kambini na kikosi cha Taifa Stars kitakachojiandaa na michuano hiyo ya Kombe la Cosafa litakalochezwa Afrika Kusini.
0 COMMENTS:
Post a Comment