June 26, 2017Na Saleh Ally
MARA nyingi sana Watanzania wamefeli katika mikataba na kama utakuwa unakumbuka tayari serikali ya Tanzania imetangaza kuchukua uamuzi wa kupitiwa upya kwa mikataba inayohusiana na madini.

Uamuzi wa serikali ni baada ya kugundua kuna tatizo, kwamba mikataba mingi inaonekana iko kwa faida ya wawekezaji tena kwa makusudi kabisa. Huku nchi ikibaki haina kitu.

Mikataba ya madini, inaonekana ina matatizo kutokana na watu kuamua mambo yawe hivyo. Kama wapo waliofanya hivyo watakuwa wale waliokuwa wanataka kujifaidisha binafsi na baada ya hapo, wawekezaji wataendelea kufaidika mara milioni.

Katika upande wa michezo na hasa mpira wa miguu, nako kuna tatizo la mikataba. Huku nako kuna makusudi pamoja na ufahamu mdogo wa wahusika, limekuwa ni tatizo kubwa sana.

Nakukumbusha kipindi hiki ndiyo cha usajili hadi hapo kitakapofungwa Agosti 6, mwaka huu. Maana yake wachezaji ndiyo kipindi ambacho wanapambana kupata maslahi katika klabu zao wanazoongeza mikataba au mpya wanazojiunga nazo.
Pamoja na kupambana kupata hayo maslahi, wachezaji wengi wamekuwa wakiingia mkenge kutokana na ufahamu mdogo wa masuala ya mikataba hasa kwa wachezaji wengi wanaotokea katika timu ndogo kwenda kujiunga na zile kubwa.

Hamu yao ya kutaka siku moja kucheza katika timu kubwa huwapeleka mbio na kuwafanya wapoteze mwendo sahihi wa umakini kabla ya kusaini mikataba hiyo. Wengi hawaisomi na ikiwezekana hawashirikishi wataalamu.

Wengi wanakwenda kusaini mikataba ambayo mingi inakuwa imeandikwa kwa Kingereza wakati lugha hiyo inawasumbua. Wanaowapa mikataba ndiyo wanaowasomea na mwisho wanakubali kusaini.

Mkataba ni mambo ya kitaalamu, mhusika anaweza kuwa na matakwa yake lakini vizuri akawa na mtaalamu hasa mwanasheria ambaye anaweza kumsomea mkataba na kumuelekeza sehemu yenye tatizo au ambayo inahitajika kuboreshwa.

Mara nyingi wachezaji wanaosaini mikataba ambayo baadaye huwabana, utawaona ni wenye furaha muda wote lakini tatizo huanza pale inapofikia wakiwa wanataka kuvunja na hasa wanapokuwa wameamua kuihama timu husika.

Tumesikia mara nyingi sana kuna wachezaji wakilalama mikataba yao kubadilishwa, lakini mwisho ikagundulika hakukuwa na jambo kama hilo, kumbe wakati anasomewa mara ya kwanza aliambiwa maelezo tofauti na kile kilichoandikwa ndani ya mkataba husika. 

Mwisho wa mkataba kunakuwa na mgogoro, hasira, kusemana vibaya na kadhalika, jambo ambalo linadhihirisha kutokuwa na utulivu au umakini wakati wa uingiaji mikataba hiyo.
Mchezaji ambaye anajitambua hawezi kusaini mkataba wake bila kumshirikisha mhusika anayeelewa masuala ya mkataba. Ndiyo maana wachezaji wengi wana mameneja ambao watafanya kazi ya kuhakikisha kila kitu kimekaa vizuri na wao wanakwenda kumalizia kwa kuangalia kidogo na kusaini.

Mambo ya kuripua wakati wa usainishwaji wa mikataba limekuwa ni jambo la muda mrefu sana na mara nyingi wachezaji wamekuwa ndiyo wahanga wakuu wa hili. Sasa ni wakati mzuri kujifunza mambo.

Kama unaingia mkataba wa kazi, haujui unakubana wapi, faida na hasara ni zipi na umeshindwa kuutambua unaeleza nini hadi unasaini, hakika ni jambo baya kabisa.
Wachezaji walio na mameneja, pia vizuri kuwa nao wanaojitambua ambao hawatafanya mambo kienyeji. Lakini mchezaji ambaye hana meneja basi ni vizuri kuwashirikisha wataalamu ambao wanaweza kutoa ushauri hata wa siku moja hadi wiki kuhusiana na mikataba.

Hakuna haja ya kuona aibu kama ukisema haujui jambo ndani ya mkataba au Kingereza hakipandi basi utaonekana haujui mambo, mshamba au haujitambui kabisa.

Vizuri kuonekana hivyo, lakini ukawa umefanya mambo yako kwa uhakika kwa kuwa mkataba ni jambo linagusa maisha na halitaenda kwa wiki na kwisha. Tukubali kubadilika na kujifunza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV