June 19, 2017Na Saleh Ally
HAKUNA anayeweza kukataa kwamba matumaini yalikuwa makubwa sana wakati Jamal Malinzi anaingia madarakani kama Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Wakati anamaliza, ninaamini hata wale waliomtetea kwa nguvu nyingi wamebaki wachache kwa kuwa zile mbwembwe za mwanzo zinaonekana zimeisha kabisa.

TFF imekuwa na malalamiko lukuki ya kiutendaji na inaonekana wengi hawakutegemea mambo yangekuwa hivyo.

Ushabiki, ushikaji, weledi duni kiuendeshaji au utendaji wa chini yamekuwa mambo ambayo yanapigiwa kelele kwa kiasi kikubwa sana.

Ukiangalia wagombea ambao wamejitokeza kuwania nafasi ya urais ambayo inashikiliwa na Malinzi inaonyesha wazi kwamba kuna tatizo ndani ya uongozi wa shirikisho hilo na hasa nafasi ya rais.

Hata jana mchana, tayari watu sita tayari walikuwa wamechukua fomu kuwania urais wa TFF. Dalili zinaonekana huenda wakaongezeka tena leo na kuna uwezekano wakafikia hata watu kumi.

Watu sita nafasi ya urais, si jambo dogo. Wazi inaonekana ni kiti kisichoogopeka tena kama ilivyokuwa hapo awali watu walijiuliza mara mbili tatu.

Wanaoingia, wengi wao ni washindani hasa, ni watu ambao wameiongoza TFF kabla ya Malinzi au watu waliokuwa katika mpira kabla ya kiongozi huyo wa sasa wa TFF.

Kwa nini wamechukua fomu kwa kasi kubwa hivi? Kwa nini wanajiamini kwamba nafasi inawafaa wao? Hilo tuwaachie katika kampeni zao watakapopata nafasi ya kujieleza.

Uhalisia maana yake wameona kiti hakikutendewa haki nao wanataka kubadilisha mambo. Hii ni kawaida katika uchaguzi lakini jiulize mara nyingine nao wana uwezo wa kufanya hayo makubwa.

Kwangu naona faraja kwamba idadi kubwa ya watu wanajiamini kugombea nafasi ya Rais wa TFF na wakati wanachukua maana yake wanaamini wana uwezo.

Ukiangalia waliochukua fomu hizo wako waliowahi kuongoza klabu kubwa kama Yanga, Simba ambazo zinaweza kuwa funzo na njia sahihi kwao kupambana na kufanya vizuri.

Wako wale ambao wamewahi pia kushika nyadhifa za juu katika shirikisho hilo. Maana yake wana uzoefu na si watu wa kusema kuwa ni wageni na wanachoomba ni kitu wanachokwenda kujifunza.

Suala linafuatia ni ustadi, ukweli na kuwa sahihi au watu wanaotaka kufanya maendeleo kwa ajili ya shirikisho, mpira wa Tanzania na Watanzania wenyewe.

Kuna ambao wanaweza wasiwe na uzoefu na shirikisho hilo lakini wakawa na nafasi ya kufanya mabadiliko. Ingawa binafsi ningependelea kuona wanaopewa nafasi ni wale wanaolenga kufanya vizuri kupitia uzoefu na moyo wa uzalendo.

Mnakumbuka, wakati anaingia Malinzi kulikuwa na kila aina ya mihemko na wengine waliamini alikuwa akionewa na wakapiga kelele za kila namna kuonyesha wanataka aingie.

Unaona leo anamaliza muda wake watu wako kimya, hakuna kelele na wengine hata kumkosoa wanashindwa kwa kuwa walipiga sana kelele wakilia kuwa anaonewa.

Tunataka mpira wa Tanzania usonge mbele, hatutaki siasa na watu kutaka kufanya TFF ni kama kampuni ya mtu binafsi na wanaweza kufanya wanachotaka.

Ushauri kwa wanaogombea, vizuri wakaamua kuchukua fomu wakiwa wamelenga hasa kufanya mabadiliko. Kama wanataka kumshinda Malinzi, basi isiwe kwa kuwa wameona tu hawezi. Badala yake inatakiwa nao wawe wamejipanga na kweli wnaaweza.

TFF ni ya Watanzania, nimekuwa nikisisitiza hili neno. Si ya mtu binafsi au kundi la watu fulani. Huenda somo hilo nililolitoa miaka nenda rudi, linaweza kutumika sasa.

Kuwa mnaotaka kuingia TFF, malengo yenu yawe kusaidia mpira wa Tanzania. Mnaotaka kuingia, basi mlenge kuleta maendeleo na si kumshinda Malinzi.


Kutofanya vizuri kwa Malinzi, kusiwafanye mkaona kila kitu rahisi katika nafasi hiyo. Kumbukeni hata yeye aliingia ikionekana ndiye atakayebadili kila kitu, mwisho wake, unaona, wote mnautaka uongozi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV