Na Saleh Ally
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi yuko mahabusu ambako anashikiliwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za matumizi mabaya ya ofisi, utakatishaji fedha na kadhalika.
Hadi sasa, Malinzi anatuhumiwa. Si ambaye amehukumiwa, basi hatupaswi kumhukumu kwa kuwa kazi hiyo ni ya mahakama ambayo mwisho baada ya kupitia njia sahihi, itatoa maamuzi kuhusiana na suala hilo.
Vema kwetu tukavuta subira na kuiacha mahakama ambayo ni mhimili unaojitegemea na unaojua nini kifanyike katika kila jambo linaloihusu.
Wakati tunaiachia mahakama na suala la Malinzi na wenzake, mimi nashukia katika suala la Kamati ya Uchaguzi wa TFF ambao umepangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu hapo mjini Dodoma. Jana kamati ya uchaguzi chini ya Mwenyekiti Wakili Revocatus Kuuli, imetangaza kusitisha zoezi la uchaguzi.
Kuuli amesema amesitisha zoezi la uchaguzi baada ya wajumbe kukiuka taratibu. Inajulikana wako waliotaka lazima Malinzi afanyiwe usaili hata kwa maandishi.
Katika wajumbe hao walitaka kwa kuwa ndiye anashikilia kiti cha urais wa TFF, apitishwe tu na kusonga katika uchaguzi. Kuuli amekataa kwa kuwa utaratibu ni lazima kila mgombea afanyiwe usaili mwenyewe na kamati hiyo.
Kinachoonekana wajumbe wako kwa ajili ya kuhakikisha Malinzi anashiriki uchaguzi tu, si kwa ajili ya kutenda haki na wamepania lazima agombee. Hii ni aibu kubwa kwa kuwa inaonyesha tulivyo.
Sasa uchaguzi umeahirishwa kwa kuwa tu inaonekana bila Malinzi mpira wa Tanzania hautakuwa na njia ya kwenda na akigombea yeye utakuwa na maendeleo kama ulivyofikia ulipo sasa.
Nilisikia mjumbe mmoja akipaza sauti kwamba wao wanne wameshinda wakitaka lazima ashiriki na mwenyekiti wao Kuuli pekee ndiye amekataa na hilo si jambo sahihi. Hakika inasikitisha sana kuona watu wanakubali kukiuka taratibu sahihi waziwazi bila ya woga.
Tena wanaokiuka wanaonyesha ubabe wa wazi wakiwa wanalazimisha jambo ambalo linajulijana wazi. Sidhani kama umewahi kusikia mtu anafanyiwa usaili eti kwa maandishi wakati inajulikana nini kinatakiwa kufanyika.
Sasa uchaguzi umesitishwa huku wale wote waliokuwa wamepita kwenye usaili wakionekana “si watu”, hawawezi “kufanya vizuri”, “si sahihi” hadi awepo mtu fulani, hii ni picha halisi ya mambo yalivyokuwa ndani ya TFF na yalivyokuwa yakipelekwa.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), wametuma wajumbe. Ninaamini watakutana na kamati ya utendaji siku itakapokaa lakini nawaasa wajumbe wa kamati ya utendaji kuwa watu makini na kuepuka kufanya mambo kama yaliyofanywa na kamati ya uchaguzi ambayo wajumbe wake wametuonyesha picha halisi.
Ushauri wangu mwingine niwakumbushe, kwamba tuko ndani ya serikali ya awamu ya tano. Mambo ya kubabaisha vitu hayawezi kuwa na nafasi hata kidogo.
Niwashauri tena wajumbe wa kamati ya utendaji kuwa makini na kutoiingilia mahakama. Huu ni mhimiliki unaojitegemea na unajua unafanya nini unapofikia wakati wa kutafuta haki.
Isije kukawa na propaganda za kisiasa ndani ya mpira kwa sababu ya kutaka kulazimisha tu mtu fulani ni lazima agombee kwa sababu ya uswahiba, utoaji shukurani au jambo fulani.
Waungwana Tanzania ni nchi yangu mimi na wewe. Kama mnaona kuna sehemu ya haki na utaratibu unajulikana, basi tutende haki. Tusiwe waumini wa kulia sehemu fulani haki haitendeki wakati sisi ni sehemu ya wakiukaji wa haki.
Kama mnataka kutenda ‘haki’ kwa mtu mmoja au kundi fulani, halafu mnaacha kutenda haki kwa wengi walioafuata taratibu sahihi, jiulizeni mara mbili na mjue mnafanya yasiyo sahihi na hamko sahihi.
Mpira wa Tanzania unaweza kuendelea bila ya kutokuwepo kwa yeyote. Mimi nimpongeze Kuuli kwa kuwa mtu anayefuata weledi na anaonyesha ni wakili aliyebobea kiutendaji kwa kuwa ametaka kutenda haki kwa kufuata utaratibu sahihi.
0 COMMENTS:
Post a Comment