July 13, 2017Inaonekana bado mambo ni magumu kwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ katika kesi inayowakabiri.

Leo wamepandishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar na kurudishwa rumande mpaka Julai 20, mwaka huu watakapopandishwa tena.

Awali viongozi hao walipandishwa mahakamani hapo Juni 29, mwaka huu na kusomewa mashitaka hayo wakidaiwa kughushi nyaraka zinazodaiwa kujilipa madeni kiasi cha dola 300,000.

Katika kesi hiyo namba 214 inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, Aveva alikutwa na kosa la kutoa nyaraka za uongo kwenye Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe jijini Dar es Salaam, Machi 10, 2016.

Kosa la tatu ni la kutakatisha fedha kinyume cha sheria ambapo inadaiwa Aveva na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo ikiwa ni kinyume cha sheria.


Katika kosa la nne, Kaburu alikutwa na shitaka la kutakatisha fedha kiasi cha 300,000 na kuziweka kwenye Benki ya  Barclays Tawi la Mikocheni jijini Dar es Salaam, huku kosa la tano la kutakatisha fedha hizo likimhusu Kaburu kutokana na kumsaidia Aveva kutakatisha fedha katika Benki ya Barclays kwa kughushi nyaraka.

Aveva na Kaburu walirudishwa rumande baada ya upande wa mashitaka ambao ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kudai haujakamilisha ushahidi wake katika kesi yenye mashitaka matano inayowakabili watuhumiwa hao yakiwemo ya utakatishaji fedha.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV